10.1 C
New York

Simbachawene: Watanzania wameonesha uzalendo kwa kudumisha amani

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, amesema Watanzania wameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa kudumisha amani na utulivu, kufuatia wito wa maandamano uliosambaa kupitia mitandao ya kijamii.

Akizungumza leo, Desemba 9, alipokuwa kwenye ziara ya kukagua hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam, Simbachawene alisema mshikamano wa wananchi umechangia kwa kiasi kikubwa kuzuia taharuki na kuvurugika kwa shughuli za kijamii na kiuchumi.

Awali, kulikuwepo taarifa za uwepo wa wito wa maandamano yaliyopangwa kupitia mitandao ya kijamii, ambayo yalidaiwa kuwa mwendelezo wa matukio ya Oktoba 29. Maandamano hayo ya awali yaliripotiwa kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa miundombinu katika baadhi ya maeneo.

“Watanzania wameonesha mshikamano, umoja na uzalendo kwa kutowasikiliza waliokuwa wakihamasisha maandamano yasiyo na ukomo,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa kazi ya vyombo vya ulinzi na usalama imekuwa nyepesi zaidi kutokana na ushirikiano mkubwa wa wananchi katika kulinda amani na utulivu wa nchi.

“Sifa na heshima iende kwa Watanzania. Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa ufanisi zaidi pale wananchi wanapokuwa tayari kulinda usalama wa nchi yao,” alisisitiza.

Waziri huyo aliwahakikishia wananchi kuwa hakuna haja ya hofu katika kuendelea na shughuli zao za kawaida, akihimiza wafanyabiashara, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kurejea kazini kama kawaida kuanzia kesho.

“Kesho watu waende kazini kama kawaida. Hakuna sababu ya kuhofia kuendelea na shughuli za kila siku,” alisema.

Pia amebainisha kuwa katika kipindi hiki kinachoelekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha doria na ulinzi, huku akiwahimiza wananchi kufanya shughuli zao kwa amani na uhuru.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img