MANILA, Ufilipino
MAHAKAMA Kuu nchini Ufilipino imemuhukumu kifungo cha maisha gerezani mwanasiasa maarufu na Meya wa zamani, Alice Guo.
Guo aliyekuwa Meya wa Bamban, ameangukiwa na hukumu hiyo baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka ya usafirishaji wa binadamu.
Guo, kwa mujibu wa taarifa, ni raia wa China lakini alipata nafasi ya Meya baada ya kujifanya raia wa Ufilipino.
Mbali ya usafirishaji wa binadamu, Guo alikuwa akiendesha kampuni ya kamari, ambayo pia inatajwa kuhusika katika matukio ya utapeli wa mitandaoni.
Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka wa Serikali, Olivia Torrevillas, Guo ni miongoni mwa raia nane wa kigeni waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Vyombo vya habari vimeifafanua hukumu hiyo vikisema ni kifungo cha miaka 40 gerezani, sambamba na faini ya Dola za Marekani 33,875.
Alikamatwa mwaka jana na vyombo vya ulinzi vya Indonesia alipoingia nchini humo akitokea Ufilipino alikokuwa akitafutwa.
Published:


