Na mwandishi wetu, Gazetini
UTAFITI mpya umeitaja Afrika Kusini kuwa ndiyo nchi ambayo wananchi wake wanatumia muda mwingi mitandaoni.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya We Are Social and Data Reportal imeeleza kuwa Waafrika Kusini hutumia zaidi ya saa tisa kwa siku wakiwa mitandaoni.
Ni kwa maana hiyo, Afrika Kusini si tu inaongoza barani Afrika, bali pia ni kinara duniani ikiwa na matumizi ya mtandao ya asilimia 72.
Itakumbukwa, asilimia 92 ya Waafrika Kusini waliohojiwa katika utafiti wa Kampuni ya Addozy mwaka jana walisema hawawezi kuwa mbali ya simu zao kwa saa 24 tu.
Pia, kati ya waliohojiwa, asilimia 64 walisema wamekuwa walipata wakati mgumu wanapokuwa mbali ya simu zao kwa muda wa saa moja tu.
Aidha, wengine asilimia 40 walisema wako tayari kuvumilia foleni ya usafi wanapokuwa njiani kwenda kazini kuliko kuwa mbali ya simu zao.
Wakati huo huo, matumizi ya mtandao kwa siku yameonekana kuwa ni madogo katika mataifa ya Nigeria, Misri na Kenya.
Kwa upande mwingine, mataifa mengine ambayo watu wake wamekuwa wakitumia muda mwingi mitandaoni ni Brazil, Ufilipino, Chile, Colombia, Argentina, Malaysia, Urusi na Falme za Kiarabu (UAE).
Hali ni tofauti na Denmark, Norway na Ujerumani, ambapo watu wake hutumia wastani wa saa tano pekee mitandaoni.
Hata hivyo, utafiti huo unaeleza kuwa kutumia muda mwingi mitandaoni hakumaanishi ustawi wa shughuli za uzalishaji.
Kwamba kati ya watumiaji 100 wanaoweza kuwa mtandaoni wakati fulani, huenda asilimia zaidi ya 50 wameingia kujifurahisha tu na si kufanya mambo ya msingi.
Kutokana na hilo, haishangazi kuona Denmark, Norway na Ujerumani, licha ya watu wake kutumia muda mchache mitandaoni, bado mataifa hayo yanafanya vizuri katika nyanja mbalimbali, zikiwamo za kiuchumi.
Published:


