New York, MAREKANI
MICHELLE Obama ambaye ni mke wa Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, amesema katika mahojiano ya hivi karibuni kwamba bado Marekani haijawa tayari kuwa na Rais mwanamke, akitolea mfano kushindwa kwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Kamala Harris, katika kinyang’anyiro cha urais mwaka jana.
“Athari za uchaguzi uliopita zinaonyesha wazi, kwa bahati mbaya, hatujawa tayari,” amesema Michelle, alipojibu swali aliloulizwa na mwigizaji Tracee Ellis Ross kuhusu kama nafasi ya kutosha imeandaliwa kwa mwanamke kuongoza taifa hilo.
Akiendelea, Michelle amesema: “Ndiyo maana huwa nawaambia, msinitazame mimi kugombea. Hamko tayari kwa mwanamke. Bado tuna safari ndefu ya kukua, na bado wapo wanaume wengi ambao hawaamini wanaweza kuongozwa na mwanamke, na tumeliona hilo.”
Mazungumzo hayo yalifanyika Brooklyn, New York, wakati wa uzinduzi wa kitabu chake kipya, “The Look,” kinachoangazia mtazamo wake kuhusu mitindo na siasa wakati yeye na Rais wa zamani Barack Obama walipokuwa Ikulu. Mazungumzo hayo yalichapishwa mtandaoni siku ya Ijumaa.

Michelle Obama amekuwa mmoja wa viongozi maarufu na wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama cha Democratic, hali iliyowafanya baadhi ya wafuasi wake kuhitaji mara kwa mara ajitose kugombea urais, jambo ambalo ameendelea kulikataa hadharani. “Sitawahi kugombea urais,” alisema mwaka 2016 akiwa bado Mama wa Taifa.
Mwaka jana, Michelle alimpigia kampeni Kamala Harris akionya kuhusu kile alichokitaja kuwa ni hatari ya kurejea kwa Donald Trump madarakani, hasa kwa afya ya wanawake.
“Tafadhali, msikabidhi hatma yetu kwa mtu kama Trump, ambaye hatuelewi na ametuonesha dharau kubwa,” alisema kwenye mkutano wa kampeni huko Michigan, siku chache kabla ya uchaguzi.
Katika mkutano huo huo, aliwauliza wananchi:
“Kwa kila kipimo, Harris ameonyesha yuko tayari. Swali la kujiuliza ni: Je, kama taifa, sisi tuko tayari kwa wakati huu?”


