Na Hassan Mwasha, Gazetini
NI rasmi sasa Mussa Hassan Zungu ndiye Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akichukua nafasi ya aliyekuwa ‘bosi’ wake katika Bunge lililopita, Tulia Ackson.
Amekalia kiti hicho na kuwabwaga wagombea wengine watano wa nafasi hiyo ya Spika wa Bunge baada ya ushindi wa kura 378 kati ya 383 zilizopigwa na wabunge.
Hivyo basi, Zungu anaingia katika historia na kuungana na wabunge wengine waliowahi kushika nafasi hiyo nyeti ya Spika wa Bunge tangu mwaka 1956.
Wengine waliowahi kukalia kiti hicho ni A.Y.A. Karimjee (1956 – 1962), Chief Adam Sapi Mkwawa (1962 – 1973 na 1975 – 1994), Chief Erasto Mang’enya (1973 – 1975), na Pius Msekwa (1994 – 2005).
Pia, orodha hiyo inawajimuhisha Samuel Sitta (2005–2010), Anne Makinda (2010–2015), Job Ndugai (2015–2022), na Dk. Tulia (2022 – 2025).
Binafsi, hanipi shaka kuona Zungu amekalia kiti hicho. Si tu kutokana na busara na uzoefu mkubwa alionao, bali pia kwa namna alivyoijenga taswira yake katika uwanja wa siasa. Yuko tofauti.
Kwa wachambuzi wa siasa, Zungu ni miongoni mwa wanasiasa wachache wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliofanikiwa kuvuna ushawishi hata mbele ya wapinzani.
Ni kutokana na mvuto huo wa kipekee, haishangazi kuona akiwa Mbunge wa Ilala kwa awamu ya tano mfululizo, ikidhihirisha wazi kuwa wanasiasa wa upinzani wamekosa namna ya kumng’oa kwenye Jimbo hilo.
Kwa upande mwingine, akiwa Spika wa Bunge kwa sasa, Zungu hawezi kukataa kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikikosolewa vikali, hasa awamu iliyopita (Bunge la 12) akiwa Naibu Spika.
Anafahamu kuwa ipo dhana kwamba wananchi wamepoteza imani yao kwa Bunge, wakiamini kuwa limechukua sura mpya ya kuitetea Serikali na si kusimamia, kuiuliza maswali magumu, kuishauri na hata kuiwajibisha.
Pili, kama ilivyokuwa Bunge la 12 akiwa Naibu Spika chini ya Dkt. Tulia, Zungu anakwenda kuongoza Bunge la ‘upande mmoja’. Bunge lililomezwa na wanasiasa wa Chama tawala, CCM.
Ni kwa maana hiyo, wachambuzi wa siasa wanaweza kutabiri kuwa hakutokuwa na minyukano mikali, labda kama ilivyokuwa katika Bunge la 11 chini ya Ndugai au Bunge la 10 lililoongozwa na Makinda.
Sasa, kuongoza Bunge lenye idadi kubwa ya wanasiasa wa upande mmoja ni jambo moja, ila kuwasimamia na kuwaweka kwenye msingi unaoakisi masilahi ya Taifa, badala ya kujipendekeza kwa Serikali, ni jambo jingine na ndilo wanalohitaji wananchi.
Kwa wananchi, Bunge ni Taasisi huru. Ni muhimili unaopaswa kujitegemea na usiohitaji ‘kutia huruma’ ili kupata hisani ya Serikali au Mahakama.
Licha ya wingi wa wabunge wa CCM, Zungu ana mtihani wa kurejesha uhai wa Bunge, ambao kwa miaka ya hivi karibuni umeondoshwa na uhusiano usio na afya kati yake na Serikali.
Kupitia Bunge la 13, matarajio ya wananchi walio wengi, ambao ‘mzuka’ wao wa kufuatilia vikao vya Bunge umepotea, tofauti na ilivyokuwa wakati wa Bunge la 10, ni kuona kiti cha Zungu kinafungua ukurasa mpya kwa masilahi mapana ya nchi
Published:


