WASHINGTON DC, Marekani
SERIKALI ya Marekani chini ya Rais Donald Trump imetangaza kusitisha misaada yake kwa Colombia, ikidai Taifa hilo halina nia ya kutokomeza uzalishaji wa dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa Rais Trump, dawa za kulevya zinazozalishwa Colombia ni chanzo cha madhara makubwa, ikiwamo vifo, kwa watu wa Marekani.
Aidha, Rais Trump amemtumia ujumbe Rais wa Colombia, Gustavo Petro, akimwambia ni bora akaendesha operesheni ya kumaliza dawa za kulevya, kabla ya Marekani kuingia nchini humo kwa lengo la kumsaidia.
Uhusiano kati ya mataifa hayo umezorota kwa miezi ya hivi karibuni na mwezi uliopita Rais Trump aliishutumu Colombia akisema haioneshi kuunga mkono mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake, Rais wa Colombia, Petro, ameinyooshea kidole Serikali ya Marekani akisema imekuwa ikiingilia masuala yake ya ndani.
Akitumia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X, Petro aliishutumu Marekani kwa mauaji ya mvuvi aliyemtaja kwa jina la Alejandro Carranza.
Carranza aliuawa katika shambulizi la Marekani nchini Colombia, wakati huo akiwa kwenye shughuli zake za uvuvi.
“Serikali ya Marekani imefanya mauaji na imekiuka mamlaka tuliyonayo katika mipaka ya majini,” amesema Petro.
Published:


