DHAKA, Bangladesh
WAENDESHA mashitaka wa Bangladesh wameomba Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Sheikh Hasina, kuhukumiwa kifo kutokana na machafuko yaliyomtoa madarakani mwaka jana.
Hasina (78), ambaye amekimbilia India, anakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu.
Katika ushahidi ulionaswa na kufikishwa mahakamani, Hasina aliagiza vyombo vya dola kutumia silaha za moto kudhibiti maandamano hayo yaliyoongozwa na wanafunzi.
Kwa wiki kadhaa za maandamano hayo, yalisababisha vifo vya watu 1,400, ingawa yalihitimisha utawala wa miaka 15 wa mwanasiasa huyo.
Wachambuzi wa siasa wanaamini kuwa hayo yalikuwa machafuko makubwa zaidi kutokea Bangladesh tangu vita ya kugombea uhuru mwaka 1971.
Kwa upande wake, Mwendesha mashitaka Mkuu, Tajul Islam, amemtaja Hasina kuwa ni kiongozi aliyekuwa na lengo la kung’ang’ania madaraka.
“Lengo lake lilikuwa ni kubaki madarakani milele, kwa ajili ya manufaa yake na familia yake,” amesema Islam kuiambia Mahakama.
Hata hivyo, Hasina amekana mashitaka yanayomkabili, huku mwanasheria wake akisema polisi walilazimika kutumia risasi za moto kutokana na nguvu kubwa waliyokuwa nayo waandamanaji.
Bangladesh itaingia katika Uchaguzi Mkuu mapema mwakani lakini Chama cha Hasina, Awami League, hakitashiriki baada ya kuzuiwa kujihusisha na siasa.
Published:


