Na mwandishi wetu, Gazetini
KWA sasa, Madagascar iko chini ya jeshi lililounda Serikali baada ya kumng’oa aliyekuwa Rais wa Taifa hilo, Andry Rajoelina. Taarifa ya jeshi kuchukua nchi ilikuja baada ya kiongozi huyo kukimbia.
Katika hotuba yake kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, Rajoelina alisema uamuzi wake wa kwenda mafichoni, ambako hata hivyo hakupataja, ulitokana na jeshi kusuka mpango wa kumuua.
Jeshi liliunga mkono maandamano makubwa ya vijana wa Madagascar waliokuwa mitaani wakishinikiza Rajoelina kujiuzulu, waliamini ameshindwa kumaliza kero nyingi zilizopo, ikiwamo ugumu wa maisha kwa wananchi walio wengi.
Ikumbukwe, kiongozi huyo alijaribu kutuliza hasira za vijana hao kwa uamuzi wake wa kumfuta kazi Waziri Mkuu na kisha kuvunja Baraza la Mawaziri, jambo ambalo hata hivyo halikuweza kuzima maandamo.
Vijana wa Madagascar walimgeukia Rajoelina na kumtaka kujiuzulu, licha ya kwamba walikuwa na imani naye alipopitishwa na jeshi kuiongoza nchi hiyo akiwa rais mwenye umri mdogo zaidi duniani (miaka 34) mwaka 2009.
Ni miaka 16 tu iliyopita, ambapo Rajoelina, licha ya kutokuwa na jina kubwa katika siasa, alikuwa na ushawishi mkubwa kwa vijana kutokana na umaarufu wake katika tasnia ya muziki akiwa ‘DJ’.
Ni wakati huo, Rajoelina alikuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Rais Marc Ravalomanana, hasa baada ya kituo chake cha televenisheni kufungiwa mwaka 2008.
Ravalomanana, ambaye alikuwa na umri wa takribani miaka 60 wakati huo, alishapoteza ushawishi wake kwa vijana wengi wa Madagascar. Kutokana na machafuko yaliyosababisha vifo vya watu 130, alikimbilia Afrika Kusini.
Vijana waliamua kuandamana mitaani wakishinikiza Ravalomanana kuachia nchi na hatimaye jeshi liliunga mkono maandamo hayo. Rajoelina akaingia madarakani kwa msaada wa jeshi, uamuzi ulioungwa mkono na vijana wengi walioamini angebadilisha maisha yao.
Ni miaka 16 imepita na sasa vijana hao wamemgeukia Rajoelina mwenye umri wa miaka 51 wakisema ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi alizoahidi wakati anaingia madarakani.
Katika maandamano hayo, vijana waliweza kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu ya usafiri, pia wakichoma moto baadhi ya majengo muhimu ya Serikali.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, vyombo vya dola vilitumia nguvu kubwa kudhibiti maandamano hayo na kusababisha vifo vya watu 22 na wengine wakiachwa na majeraha.
Historia yake
Rajoelina, ambaye taarifa za ndani zinaeleza kuwa amekimbilia nchini Ufaransa, alizaliwa mwaka 1974, mjini Antisirabe. Baba yake alikuwa kanali wa jeshi la Madagascar.
Kabla ya kuingia katika siasa na hatimaye kuwa Meya mwaka 2007, aliwahi kuwa ‘DJ’, kabla ya kununua moja ya vituo vya redio n baadaye kumiliki kituo cha televisheni.
Wakati wa janga la Corona, Rajoelina atakumbukwa kwa kitendo chake cha kuibuka na dawa ya kienyeji aliyodai ingeponyesha mgonjwa ndani ya siku tatu tu baada ya kuitumia. Haikuwa hivyo.
Baada ya kuingia madarakani kwa nguvu ya jeshi lililompindua Ravalomanana mwaka 2016, Rajoelina aling’atuka mwaka 2014, kabla ya kurejea Ikulu aliposhinda kupitia Uchaguzi wa mwaka 2018.
Mwaka 2023, alishinda tena kiti cha urais, ingawa safari hii kulikuwa na maandamano makubwa yaliyozuka baada ya wapinzani kuja juu wakidai Uchaguzi ulitawaliwa na ‘figisu’ nyingi. Pia, walidai Rajoelina hakustahili kugombea kwa kuwa tayari alishachukua uraia wa Ufaransa.
Ugumu wa maisha, Rushwa
Miongoni mwa ahadi hizo ni kuboresha hali ya maisha lakini takwimu zilizopo hazioneshi kupungua kwa kiwango cha umasikini miongoni mwa wananchi wa kipato cha chini.
Takwimu za Benki ya Dunia zinaonesha kuwa asilimia 80 ya raia milioni 31 wa Madagascar wanaishi kwenye umasikini, ikiwamo kushindwa kumudu gharama za chakula.
Aidh, ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa inaeleza kuwa ni asilimia ndogo tu ya wananchi wanaotumia nishati ya umeme. Ni wakati huo huo, Shirika lao la umeme linakabiliwa na kashfa kadhaa za rushwa.
Wakati huo huo, vijana wa Madagascar wanalalamikia ugumu wa kupata ajira na uhaba wa huduma za kijamii, hasa maji na umeme. “Tulimpa muda wa kutosha. Maisha ya hapa Madagascar ni magumu… Tunahitaji mtu atakayeshughulika na matatizo yetu,” alisema mmoja ya waandamanaji hao.
Licha ya ugumu wa maisha kwa wananchi, Serikali ya Rajoelina imekuwa na kashfa nyingi za rushwa. Takwimu zinaitaja nchi hiyo kushika nafasi ya 118 Kati ya 140 zenye kiwango cha juu cha rushwa.
Mwaka jana, Mahakama mjini London, Uingereza, ilimfungulia mashitaka aliyekuwa mtumishi wa Serikali ya Rajoelina ikidai alilipwa kiasi kikubwa cha fedha ili kuipa kampuni moja haki ya kuchimba madini nchini Madagascar.
Katika hilo la rushwa, vijana wa Madagascar wanamtaja mfanyabiashara maarufu, Maminiaina Ravatomanga, kuwa Ni miongoni mwa wanaopaswa kufunguliwa mashitaka na kuhukumiwa. Huyo ni miongoni mwa watu wa katibu wa Rajoelina.
Kwa ufupi, vijana hawajaiona tofauti ya Rajoelina na mtangulizi wake, Ravalomanana, licha ya matarajio makubwa waliyokuwa nayo kwa kijana mwenzao huyo miaka 16 iliyopita.
Kanali aapishwa, aanza kazi
Kiongozi wa jeshi, Kanali Michael Randrianirina, alipishwa jana, muda mfupi tu baada ya kutangaza kupitia matangazo ya redio kuwa ataiongoza nchi kwa sasa, na kisha Uchaguzi wa kupisha Serikali ya kiraia utafanyika miaka miwili baadaye. “Tumeitikia sauti ya watu, hatujapindua Serikali,” amesema Randrianirina baada ya kuapishwa.
“Leo ni mwanzo wa historia mpya katika historia ya nchi yetu hii. Tuna furaha kuanza ukurasa mpya wa maisha ya taifa letu.”
Katika hatua yake ya kwanza, hata kabla ya kuapishwa, Randrianirina alivunja taasisi zote za Kidemokrasia, ikiwamo Tume ya Uchaguzi na Mahakama ya Katiba, akiliacha Bunge ambalo lilipiga kura ya kumtoa madarakani Rais wao, Rajoelina.
Kwa upande mwingine, hatua hiyo ya jeshi kuchukua nchi imeungwa mkono pia na Waziri wa Ulinzi, Manantsoa Deramasinjaka Rakotoarivelo, ambaye amesema: “Ninawapa baraka zangu zote.”
Hata hivyo, kwa miaka mingi, tangu Madagascar ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960, siasa za nchi hiyo zimekuwa zikitawaliwa na utamaduni wa jeshi kuingia Ikulu na kushika dola.
Published:


