Na Samwel Mwanga, Maswa
KATIKA jamii nyingi za vijijini nchini Tanzania, hususan katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, masuala ya haki ya uzazi na ukatili wa kijinsia bado ni changamoto kubwa kwa wanawake na wasichana.
Licha ya juhudi mbalimbali za Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wanawake wengi bado hukumbana na vikwazo vya kijamii, kiutamaduni na kiuchumi vinavyowazuia kufanya maamuzi huru kuhusu afya yao ya uzazi.
Makala hii inaangazia hali halisi ya huduma za uzazi wa mpango, mitazamo ya kijamii, ukatili wa kijinsia unaohusiana na maamuzi ya uzazi, pamoja na juhudi zinazofanyika kuleta mabadiliko.
Uelewa kuhusu huduma za uzazi wa mpango
Uchunguzi wa mahojiano unaonyesha kuwa wanawake wengi vijijini wana uelewa wa kimsingi kuhusu huduma za uzazi wa mpango na wanazitambua njia mbalimbali kama vile vidonge, sindano, vipandikizi na kondomu.
Vyanzo vya elimu ni pamoja na kliniki za afya, kampeni za mashirika ya afya na vipindi vya redio za kijamii.
Holo Machibya, mkazi wa kijiji cha Mwamanenge, alisema alipata taarifa kuhusu huduma hizo kupitia kliniki ya kijiji na kampeni za afya zilizofanywa na Shirika la World Vision Tanzania.
“Wauguzi walieleza njia mbalimbali kama vidonge, sindano, vipandikizi na kondomu. Pia niliwahi kusikia kupitia redio Sibuka FM kuhusu umuhimu wa kupanga uzazi kwa afya ya mama na mtoto,” alisema.
Aliongeza kuwa licha ya uelewa huo, hakutumia huduma hizo kutokana na hofu ya madhara ya kiafya kama kutopata hedhi au kuongezeka uzito, na pia mume wake hakupenda atumie njia yoyote akiamini ni sawa na kuzuia mapenzi ya Mungu.
Sophia Khija, mkazi wa kijiji cha Nghami, alisema mume wake alikuwa na mtazamo hasi kuhusu kupanga uzazi, akiamini ni njia ya kupoteza maadili na kwamba angetumia nafasi hiyo kufanya mambo yasiyofaa.
“Aliona watoto kuwa baraka na alitaka tuzae kadri Mungu atakavyotoa. Ndugu zangu wengine walikuwa na mitazamo tofauti; dada yangu mkubwa ambaye ni mwalimu alinisaidia kuelewa umuhimu wake, lakini wengine waliona ni kinyume na mila za Kisukuma,” alisema.
Dorotea Gwisu, mkazi wa kitongoji cha Bugarama, alisema mume wake alimzuia kutumia njia ya uzazi wa mpango na kumtishia kumfukuza nyumbani.
“Alininyanyasa kwa maneno makali na kunizuia kwenda kliniki. Nilihisi kukandamizwa, hasa nilipokuwa nafikiria afya yangu na watoto wetu wanne ambao wamekuwa wakizaliwa kila baada ya miaka miwili,” alisema.
Hata hivyo, licha ya uelewa huo, matumizi ya huduma hizo bado ni duni kutokana na hofu ya madhara, imani potofu na mitazamo hasi kutoka kwa waume au jamii kwa ujumla.
Mitazamo ya wanaume na familia
Mitazamo ya wanaume ina mchango mkubwa katika uamuzi wa mwanamke kuhusu matumizi ya uzazi wa mpango.
Shija Malale, baba wa watoto sita kutoka kijiji cha Bukigi, alisema kupanga uzazi kunapingana na mipango ya Mungu.
“Biblia inasema ‘nendeni mkazaane na mkaijaze dunia,’ hivyo kuleta masuala ya uzazi wa mpango ni kama kupingana na mpango wa Mungu,” alisema.
Baadhi ya wanaume huenda mbali zaidi kwa kutumia lugha za matusi, vitisho au hata kuwazuia wake zao kutafuta huduma za uzazi.
Hata pale ndugu wa karibu wanapojaribu kutoa ushauri, sauti zao mara nyingi hulemazwa na nguvu ya mfumo dume na mila zilizokita mizizi.
Ukatili wa kijinsia na maamuzi ya uzazi
Matukio ya ukatili wa kijinsia unaohusiana na maamuzi ya uzazi ni ya kawaida, lakini hayaripotiwi mara kwa mara.
Wanawake wanaotaka kutumia njia za kupanga uzazi hukumbana na unyanyasaji wa maneno, kushurutishwa kuacha huduma hizo, au kunyimwa ruhusa ya kuhudhuria kliniki.
“Ukatili huu huathiri siyo tu afya ya mwanamke, bali pia ustawi wa familia,” alisema Esther Jidamabi, mkazi wa kijiji cha Gulungwashi.
Changamoto katika upatikanaji wa huduma
Katika maeneo mengi ya vijijini, zahanati ni chache na ziko mbali na makazi ya watu.
Mara nyingi hukabiliwa na ukosefu wa vifaa muhimu kama damu salama, dawa kama oxytocin, na vifaa vya kufuatilia afya ya mama na mtoto. Wahudumu wa afya pia ni wachache, na wengine hukosa mafunzo ya utoaji huduma kwa heshima na usawa wa kijinsia.
Kulwa Ngolongo, mkazi wa kijiji cha Likungulyankoma, alisema:
“Huduma za afya ni za kiwango cha kati. Hakuna zahanati ya serikali, hivyo tunatembea takriban kilomita nane kufuata huduma kijiji cha Senani. Wakati wa mvua barabara ni mbaya sana, na mara nyingi hakuna dawa za uzazi wa mpango,” alisema.
Mikakati ya kuwezesha wanawake
Elimu kuhusu haki za afya ya uzazi kwa wanawake na wanaume wote ni muhimu.
Huduma za afya zinapaswa kuboreshwa kwa kuweka vituo karibu na wananchi, kuwa na vifaa vya kutosha na wahudumu waliopata mafunzo ya utoaji huduma kwa heshima.
“Elimu iende sambamba na utekelezaji wa sheria za kulinda wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia. Wanawake wapewe nafasi ya kufanya maamuzi kuhusu miili yao bila hofu,” alisema Elizabeth Musi, Afisa Maendeleo ya Jamii.
Wataalamu wa afya wanasemaje?
Ndebile Mboje, Afisa Tabibu Msaidizi katika zahanati ya Budekwa, alisema asilimia 40 hadi 50 ya wajawazito wanaofika zahanatini hapo huwa wamepanga mimba zao.
“Hata hivyo, bado kuna idadi kubwa ya wanawake — hasa wa umri mdogo — ambao mimba zao hazijapangwa kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi na hofu ya mitazamo ya kijamii,” alisema.
Aliongeza kuwa uhaba wa damu salama, dawa aina ya Oxytocin, na vifaa vya kufuatilia mapigo ya moyo ya mtoto tumboni huongeza hatari ya vifo vya mama na mtoto, hasa pale ambapo hakuna huduma ya rufaa ya haraka.
Wilaya na mikakati ya dharura za uzazi
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Hadija Zegega, alisema kuwa huduma za afya za uzazi katika vijiji bado zinakabiliwa na changamoto za vifaa na rasilimali watu.
“Mara nyingi tunatoa huduma za awali na kisha kuwapeleka wagonjwa hospitali ya wilaya. Changamoto nyingine ni ucheleweshaji wa maamuzi kutoka kwa familia, ukosefu wa magari ya wagonjwa na ubovu wa barabara hasa wakati wa mvua,” alisema.
Mikakati ya halmashauri ya wilaya
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, alisema halmashauri imeweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango vijijini kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi.

“Tunashirikiana na mashirika kama KASODEFO kutoa elimu kuhusu afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto, na uzazi wa mpango,” alisema.
Aidha, zahanati na vituo vya afya vinapanga kliniki za uzazi wa mpango na kutoa elimu ya afya kupitia mikutano ya kijamii na viongozi wa vijiji.
Kauli ya mkuu wa wilaya
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Vicent Naano Anney, alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeimarisha sera na mikakati ya kusambaza vifaa vya afya, kuongeza watumishi vijijini na kuimarisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto.

“Kwa sasa kumekuwa na ongezeko la uelewa kuhusu haki za wanawake na wasichana, hasa katika masuala ya uzazi wa mpango na ukatili wa kijinsia,” alisema. Haki ya uzazi na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ni jukumu la pamoja kati ya Serikali, jamii na mashirika ya kiraia. Haki ya mwanamke kufanya maamuzi kuhusu mwili wake si tu suala la afya, bali ni msingi wa haki za binadamu. Mabadiliko yanawezekana kupitia elimu, usawa, heshima na mshikamano wa kijamii.


