WASHINGTON DC, Marekani
RAIS wa zamani wa Marekani, Joe Biden, ameanza matibabu ya saratani ya tezi dume aliyogundulika kuwa nayo tangu Mei, mwaka huu. Kwa mujibu wa Msemaji wake, Biden ameanza rasmi kupokea tiba ya mionzi, pia akipata matibabu ya homoni.
“Kama ulivyo utaratibu wa matibabu ya saratani ya tezi-dume, Rais Biden kwa sasa anafanyiwa matibabu ya mionzi na homoni,” imeeleza taarifa ya Msemaji wake huyo. Aidha, taarifa zingine, kama zilivyoripotiwa na kituo cha televisheni cha NBC, zinaeleza kuwa matibabu ya mionzi yatachukua walau wiki tano.
Mwezi uliopita, Biden ambaye atatimiza umri wa miaka 83 mwezi ujao, alifanyiwa upasuaji wa kuondosha seli za saratani katika ngozi.
Biden aliondoka Ikulu Januari, mwaka huu, na kumpisha Donald Trump lakini anabaki kuwa ndiye rais mwenye umri mkubwa zaidi kuiongoza Marekani.
Kutokana na afya yake kutokuwa imara, alishindwa kugombea tena kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, hivyo aliyekuwa Makamu wa Rais wake, Kamala Harris, aliingia kwenye kinyang’anyiro dhidi ya Trump.


