18.1 C
New York

‘Bluetoothing’ yageuka janga Fiji, maambukizi ya VVU yaongezeka mara kumi

Published:

Suva, FIJI

Fiji sasa inakabiliwa na mlipuko mkubwa wa Virusi vya Ukimwi (VVU), huku wataalamu wakionya kuwa nchi hiyo iko katika “dhoruba kamili” ya kiafya kutokana na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya kwa sindano na tabia hatarishi inayojulikana kama bluetoothing.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, kufikia mwaka 2024 visa vya maambukizi viliongezeka hadi watu 5,900, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara kumi ikilinganishwa na miaka iliyopita. Kati ya hao, 1,583 waliripotiwa mwaka huo pekee, wengi wakiwa vijana walio chini ya miaka 20.

Naibu Waziri wa Afya wa Fiji, Penioni Ravunawa, alionya Januari 2025 kuwa idadi ya watu walioambukizwa inaweza kufikia 3,000 mwishoni mwa mwaka huu, akisema taifa hilo “linakabiliwa na hali ya dharura ya VVU.”

Chanzo kikuu cha ongezeko hilo ni matumizi ya dawa za kulevya kwa sindano na tabia hatarishi ya bluetoothing ambapo mtumiaji wa dawa hujidungia sindano, kuvuta damu yake, kisha kuinyunyiza kwa wengine. Tendo hilo mara nyingi hufanywa kwa zamu na kundi moja la watumiaji, likiwa chanzo kikuu cha maambukizi mapya.

“Niliona sindano moja ikitumiwa na watu saba kwa zamu,” anasema Kalesi Volatabu, Mkurugenzi wa Drug Free Fiji. “Wanashiriki si tu sindano, bali damu pia.”

Hali hii imeongezeka kutokana na ukosefu wa sindano mpya na gharama kubwa za dawa, huku maduka mengi yakizuia uuzaji wa vifaa hivyo.

Aidha, tabia ya chemsex matumizi ya methamphetamine kabla au wakati wa ngono — imetajwa kuwa kichocheo kingine kikubwa cha maambukizi. Watumiaji wengi nchini Fiji huichoma dawa hiyo kwa sindano badala ya kuvuta, jambo linaloongeza hatari ya kuambukizwa.

Sesenieli Naitala, mwanzilishi wa Survivor Advocacy Network, anasema tatizo limeongezeka kwa kasi kubwa miongoni mwa vijana.
“Wazee wengi wameanza kutumia dawa, lakini kinachotia hofu zaidi ni kuona vijana wadogo — hata wa miaka kumi — wakiambukizwa,” anasema. “Tulianza kutoa msaada mwaka 2013, na kijana niliyemwona miaka hiyo sasa ni miongoni mwa mamia walioambukizwa kupitia sindano.”

Mashirika kama lile la Naitala na Volatabu yamekuwa mstari wa mbele kutoa elimu, kusambaza kondomu na kuhimiza upimaji wa hiari, lakini upinzani wa kijamii na wa kidini umezuia juhudi za kuanzisha programu rasmi za “sindano salama.”

Kwa zaidi ya miaka 15, Fiji imekuwa njia kuu ya kusafirisha crystal meth katika eneo la Pasifiki, kutokana na nafasi yake kati ya Asia na Amerika. Dawa hizo sasa zimeenea ndani ya jamii, zikisababisha ongezeko kubwa la watumiaji wa sindano.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 48 ya maambukizi mapya yanatokana na matumizi ya sindano, asilimia 47 kutokana na ngono isiyo salama, huku maambukizi kutoka mama kwenda kwa mtoto yakiongoza kwa watoto walio chini ya miaka 15.

Serikali ya Fiji imeanza kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama Global Alert and Response Network kuimarisha uchunguzi na matibabu ya VVU. Hata hivyo, uhaba wa watumishi wa afya, vifaa vya maabara na upungufu wa dawa bado ni changamoto kubwa.

Mtaalamu wa usalama wa kikanda katika Chuo Kikuu cha Canterbury, José Sousa Santos, anaonya kuwa ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa haraka, Fiji inaweza kushuhudia janga la kiafya “lisilokuwa na mfano katika historia yake.”

“Tatizo si tu kile kinachoonekana sasa,” anasema. “Bali ni nini kitatokea miaka mitatu ijayo wakati mfumo wa afya utakaposhindwa kuhimili wimbi jipya la maambukizi.”

Kwa sasa, mashirika ya kijamii yanaendelea kutoa elimu na kusaidia walioathirika, huku Serikali ikikabiliwa na jukumu kubwa la kuokoa taifa lililo katika njia panda ya mlipuko wa VVU unaoongezeka kwa kasi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img