18.1 C
New York

Udumavu kwa watoto wapungua nchini

Published:


Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kiwango cha udumavu miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano nchini kimepungua kutoka asilimia 48 mwaka 1992 hadi asilimia 30 mwaka 2022.

Akizungumza Septemba 30, 2025, wakati wa kufunga Mkutano wa 11 wa Wadau wa Lishe uliofanyika katika ukumbi wa APC, Bunju, Jijini Dar es Salaam, Majaliwa alisema kiwango cha ukondefu pia kimeshuka kutoka asilimia 5 mwaka 1992 hadi asilimia 3.2 mwaka 2022.

Majaliwa alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inatambua lishe kama nguzo ya afya, uchumi na maendeleo ya watu. “Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na chakula cha kutosha, afya njema na lishe bora,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu alieleza kuwa jitihada hizo zimemwezesha Rais Samia kupata Tuzo ya Global Goalkeeper kutoka Gates Foundation kutokana na mchango wake katika kupambana na utapiamlo na kuimarisha afya ya mama na mtoto.

Hata hivyo, Majaliwa alisema changamoto imejitokeza katika ongezeko la uzito uliozidi miongoni mwa wanawake wa umri wa kuzaa, kutoka asilimia 28 mwaka 2015 hadi asilimia 37 mwaka 2022, akihusisha hali hiyo na mabadiliko ya ulaji na mtindo wa maisha.

Waziri Mkuu alizitaka wizara, taasisi na sekta binafsi kutenga rasilimali kwa afua za lishe, na vyuo vya elimu ya juu kuendeleza tafiti zitakazosaidia kuboresha sera na mikakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwan Kikwete, alisema Serikali itaendelea kuhakikisha kila wizara inajumuisha masuala ya lishe kwenye mipango ya kibajeti kila mwaka, huku akibainisha kukamilika kwa utafiti wa gharama za utapiamlo ambao utasaidia kuwashawishi watunga sera kuongeza hatua za kukabiliana na changamoto hiyo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img