15.5 C
New York

Serikali Nigeria imeshindwa vita dhidi ya Boko Haram?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
NI wazi sasa Serikali ya Nigeria inahitaji mkakati mpya wa kukabiliana na Boko Haram baada ya Kundi hilo la waasi kuua watu zaidi ya 500 katika miezi ya hivi karibuni.
Ripoti ya Taasisi ya Good Governance Africa ya Afrika Kusini inaeleza kuwa Boko Haram imeanzisha tena mashambulizi yake ya kikatili baada ya ukimya wake wa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Nigeria, watu zaidi ya 2,266 wamepoteza maisha kwa kipindi cha miezi sita tu iliyopita. Vifo vingi zaidi, ukilinganisha na takwimu za mwaka jana.
Wakati huo huo, ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) inaeleza kuwa watu zaidi ya 40,000 wamepoteza maisha na wengine takribani milioni mbili wamekimbia makazi yao tangu Boko Haram ilipoanzisha operesheni zake miaka 15 iliyopita.
Kwa upande mwingine, mafanikio hayo ya Boko Haram katika siku za karibuni yanahusishwa moja kwa moja na nguvu ndogo iliyobaki katika kukabiliana na Kundi hilo.
Machi, mwaka huu, Serikali ya Niger ilitangaza kujitoa katika Umoja wa MNJTF unaopigana na Boko Haram. Ni Umoja ulioanzishwa na Nigeria mwaka 1994 ukizihusisha pia nchi jirani za Cameroon, Chad na Benin.
Niger ilieleza kuwa uamuzi wake wa kujitoa ni kuipa nafasi ya kuelekeza nguvu katika changamoto zake za ndani za kiusalama.
Ikumbukwe, Niger haijawa na utulivu wa kutosha tangu Serikali iliyopo madarakani ilipofanya mapinduzi ya kijeshi ya kumng’oa madarakani Rais Mohamed Bazoum.
Wachambuzi wa siasa wanaamini Niger kujitoa kumeiongezea nguvu Boko Haram katika maeneo ya mpakani kati yake na Nigeria.
Licha ya mamlaka za Nigeria kusema zimerejesha utulivu katika maeneo mengi, mambo ni tofauti kwa mujibu wa wananchi.
“Watu bado wana hofu, unaweza kuona walivyo na presha. Watu bado wanashambuliwa, ni ngumu kuendesha gari nyakati za usiku, huwezi kupata usingizi. Serikali ina kazi kubwa ya kufanya,” anasema mmoja ya wananchi walihojiwa na DW.
Akisisitiza zaidi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kukabiliana na Ugaidi Magharibi mwa Afrika (WACCE), Mutaru Mumuni Muqthar, anasema:
“Ni kweli tumeona jitihada kubwa za Serikali ya Nigeria, lakini kuibuka upya kwa mashambulizi ya Boko Haram kunaibua hofu kubwa kwa wananchi.
“Kwa sasa, hakuna dalili kuwa Serikali imeweza kudhibiti vurugu za Boko Haram, pia huoni Kundi hilo likimalizwa hivi karibuni,” anasema.
Naye mchambuzi Malik Samuel anashauri kuwa namna nyingine bora ya Serikali kukabiliana na Boko Haram ni kushirikisha viongozi wa dini.
“Serikali inapoandaa mkakati, isiwaache nyuma viongozi wa dini. Msingi wa Boko Haram ni masuala ya imani,” anasema.
Ifahamike kuwa hoja ya msomi huyo inatokana na kile wanachopigania Boko Haram, kutaka sheria za Dini ya Uislam (Sharia) zitumike katika uongozi wa Taifa hilo.
Pia, Malik anasema vijana wengi wanaojiunga na Boko Haram au vikundi vingine vya waasi hushawishika kufanya hivyo kutokana na msukumo wa ugumu wa maisha.
“Mikakati ya kukabiliana na waasi, wakiwamo Boko Haram, iende sambamba na kuboresha hali ya maisha, hasa kwa vijana, ambao ni rahisi kumshawishika wanapopata ahadi za maisha mazuri wanaojiunga na uasi,” anasema Malik.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img