10.9 C
New York

Chikomo, Dk. Otaru waibeba Tanzania mapambano dhidi ya ukame, mmomonyoko wa ardhi

Published:

Wakiwa viongozi wa JET, sasa wanaiwakilisha Tanzania katika nafasi za juu za Umoja wa Mataifa chini ya mkataba wa UNCCD.

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Tanzania imeendelea kung’ara katika jukwaa la kimataifa baada ya kupata wawakilishi wake katika nafasi za juu za Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (UNCCD).

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo, ameteuliwa kuwa Mratibu wa Kitaifa kwa upande wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO National Coordinator) wa UNCCD kwa Tanzania, nafasi itakayoiwezesha nchi kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mikataba na ajenda zinazolenga kukabiliana na changamoto za mmomonyoko wa ardhi na ukame.

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo.

Akizungumza na www.gazetini.co.tz baada ya uteuzi huo, Chikomo amesema Mkataba huu ni kati ya Mikataba mitatu iliyopitishwa kwenye mkutano wa Mazingira na Maendeleo (The United Nations Conference on Environment and Development-UNCED uliofanyika nchini Brazil mwaka 1992 na kwamba Tanzania kama mwanachama imekuwa ikitekeleza majukumu yake kupitia mipango kazi ya muda mfupi, wa kati na mrefu, ikilenga kupunguza kasi ya mmomonyoko wa ardhi na athari za ukame.

“Tanzania imeendelea kutekeleza majukumu yake kama nchi mwanachama wa Mkataba katika Nyanja mbalimbali. Katika kutekeleza majukumu chini ya Mkataba, mwongozo na makubaliano ya nchi wanachama (COP Decisions), nchi wanachama zinapaswa kuandaa mpango kazi wa utekelezaji na hili linasisitizwa katika kifungu cha 9 (1) cha Mkataba (Article of the Convention),” amesema Chikomo na kuongeza kuwa:

“Lengo la Mpango kazi huu ni kuainisha visababishi vya kuenea kwa hali ya jangwa na kubuni njia muafaka za kupambana na visabishi hivyo na madhara yake hususan ukame. Tanzania iliandaa Mpango kazi wa Kitaifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame na kufanyiwa mapitio,”.

Amesema utekelezaji wa Mpango Kazi huo umegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni muda mfupi, muda awa kati na muda mrefu (1-2/3-5 na >5) huku majukumu ya utekelezaji yakiwa yametolewa katika ngazi zote za kiutendaji (Wizara za Kisekta, Mashirika ya Kiserikali, Asasi zisizo kuwa za Serikali, Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo.

Akigusia mafanikio ya utekelezaji wa mpango huo Chikomo amesema kuwa yameonekana katika nyanja mbalimbali.

“Mafanikio ya utekelezaji wa mpango kazi huu yameonekana katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa mfano; utekelezaji wa Programu ya Shabaha za kupunguza uharibifu wa ardhi (land Degradation Neutrality-Target Setting). Katika kutekeleza program hii, Tanzania tayari imeandaa na kukamilisha shabaha za kupunguza uharibifu wa ardhi katika sekta mbalimbali,” amesema.

Wakati huohuo, Dk. Ellen Otaru, Mwenyekiti wa JET, amechaguliwa kuwa Mwakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) Barani Afrika, nafasi atakayohudumu hadi kufanyika kwa Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama (COP 17).

Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru.

Dk. Otaru amesema uteuzi huo ni heshima kubwa kwa Tanzania:
“Nafasi hii si yangu pekee bali ni ya nchi nzima. Tunayo fursa ya kuonesha mchango wa Tanzania katika mapambano ya kimataifa dhidi ya uharibifu wa ardhi na ukame, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kiraia barani Afrika.”

Wanahabari na wadau wametakiwa kutumia nafasi hizi kutangaza mafanikio ya Tanzania kupitia vyombo vya habari na kufuatilia taarifa pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia tovuti rasmi ya UNCCD.

hakuna shaka kwamba uteuzi wa viongozi hao wawili kutoka JET waibua nafasi ya Tanzania kushiriki moja kwa moja katika maamuzi ya kimataifa ya uhifadhi wa mazingira na mapambano dhidi ya mmomonyoko wa ardhi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img