22 C
New York

Tanzania yapoteza hekta 460,000 za misitu kila mwaka, sheria zatajwa

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

TANZANIA inakabiliwa na ongezeko kubwa la upotevu wa misitu, hali inayochochea ukame, kukauka kwa vyanzo vya maji na kuharakisha mabadiliko ya tabianchi. Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), zaidi ya hekta 460,000 za misitu hupotea kila mwaka kutokana na uvunaji holela wa miti, matumizi makubwa ya kuni na mkaa pamoja na udhaifu katika utekelezaji wa sheria.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa licha ya kuwapo kwa Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 (iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022) pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 (marekebisho ya 2025), changamoto kubwa imekuwa kutokuzisimamia ipasavyo. Matokeo yake ni ongezeko la uharibifu wa mazingira, huku jamii nyingi zikiendelea kutegemea misitu kwa shughuli za kila siku bila kuzingatia athari za muda mrefu.

Athari za uharibifu

Kupotea kwa misitu kumechangia kupungua kwa vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali ya nchi, hali inayoongeza hatari ya ukame na kupungua kwa uzalishaji wa chakula. Wataalamu wa mazingira wanaonya kuwa bila kuchukua hatua za haraka, Tanzania inaweza kuingia kwenye mgogoro wa maji na chakula, jambo linaloweza kudhoofisha ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi.

Takwimu zinaonyesha kuwa changamoto hii si ya Tanzania pekee. Bara la Afrika lilipoteza zaidi ya hekta milioni 3.9 za misitu kati ya mwaka 2010 na 2020, ambapo Tanzania ilichangia asilimia 12 ya upotevu huo. Hii inaifanya nchi kuwa miongoni mwa maeneo yenye viwango vya juu vya ukataji miti barani Afrika.

Kauli ya wataalamu

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), ofisi ya Tanzania, Joan Itanisa, anasema tatizo la uharibifu wa misitu limekuwa na sura pana zaidi. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2019, Tanzania inapoteza takribani mikoko 479 kila mwaka, sawa na asilimia sita ya jumla ya mikoko yake.

“Mikoko hii ina mchango mkubwa katika kuhifadhi ikolojia ya pwani, kulinda viumbe vya baharini na kupunguza madhara ya mmomonyoko wa ardhi. Lakini kila mwaka tunaendelea kupoteza sehemu kubwa yake. Aidha, zaidi ya nusu ya vyanzo vya maji vimeanza kukauka, na mmomonyoko wa udongo unakadiriwa kufikia asilimia 61 ya ardhi yote nchini,” amesema Joan.

Mikakati ya kurejesha uoto wa asili

WWF kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa imezindua mpango wa “2030 Restoration Agenda” wenye lengo la kurejesha uoto wa asili na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Joan anasema kuwa mpango huo unakadiriwa kugharimu dola za Marekani trilioni 13.

“Kiasi hiki cha fedha kikitolewa, tunaamini zaidi ya hekta bilioni 18 za miti zitarejeshwa duniani, na takribani watu bilioni 4.5 watanufaika kupitia ajira, uhifadhi wa mazingira na kupungua kwa athari za mabadiliko ya tabianchi. Nchi 193 zinatarajiwa kushiriki kwa kutunga sera, kuanzisha miradi ya kitaifa na kuboresha mifumo ya kilimo na chakula,” alifafanua.

Wataalamu wanasema hali ya sasa inahitaji hatua za dharura. Serikali inapaswa kuimarisha usimamizi wa sheria zilizopo, kudhibiti uvunaji haramu wa miti na kuweka mifumo ya uwajibikaji ili kuhakikisha rasilimali za misitu zinatumika kwa tija na uendelevu. Pia, jamii zinahimizwa kubadili mitindo ya matumizi ya nishati kwa kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, na badala yake kuwekeza kwenye nishati safi na rafiki kwa mazingira.

Kwa ujumla, changamoto ya upotevu wa misitu ni kengele ya tahadhari kwa Tanzania na dunia kwa ujumla. Bila hatua madhubuti, vizazi vijavyo vitaishi katika mazingira yasiyo na usalama wa maji, chakula wala hewa safi. Hatua za sasa za kurejesha uoto wa asili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni msingi wa kulinda maisha ya binadamu na viumbe hai wote.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img