Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Mwani ni zao la baharini lenye thamani kubwa duniani. Kwa miongo kadhaa, wakulima wa mwani hususan visiwani Zanzibar na mikoa ya pwani kama Tanga, Bagamoyo, Mtwara na Lindi wamekuwa wakilitegemea kama chanzo kikuu cha mapato. Mwani hutumika katika sekta mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa dawa, vipodozi, mbolea, chakula, sabuni na hata bidhaa za viwandani zinazohusisha kemikali za asili.
Kwa Tanzania, zao hili limechangia pato la taifa kwa mauzo ya nje na kutoa ajira kwa maelfu ya wanawake na vijana. Hata hivyo, changamoto za mbinu za kienyeji, ukosefu wa masoko ya uhakika na uongezaji thamani mdogo zimekuwa kikwazo kwa wakulima kupata faida kubwa zaidi.
Katika hatua ya kulipandisha thamani zao hilo, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imezindua mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wakulima wa mwani. Mafunzo hayo yamefanyika wilayani Mkinga mkoani Tanga, yakilenga kuongeza uzalishaji, usalama na ufanisi wa kilimo.

Naibu Katibu Mkuu, Dk. James Kilabuko, akifunga mafunzo hayo, alisema: “Mafunzo ya kilimo bora cha mwani yatawasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji na ubora wa mwani katika soko la ndani na nje ya nchi. Uongezaji thamani, matumizi sahihi ya kemikali, vifungashio bora na upatikanaji wa masoko vitawapa nafasi kubwa zaidi ya ushindani,” alisema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa elimu ya huduma ya kwanza na uokoaji majini. “Mazingira ya kazi zenu ni katika maji, hivyo kujua namna ya kujiokoa ni muhimu sana. Elimu hiyo itasaidia kuokoa maisha yako binafsi na jirani yako shambani,” aliongeza.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Menejimenti, Kanali Selestine Masalamado, alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya awamu ya pili ya utekelezaji wa mwongozo wa kuimarisha ulinzi na usalama baharini na maziwa makuu uliyozinduliwa Februari 2023 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Awamu ya kwanza ilitekelezwa Mafia, Pangani na Bagamoyo kwa kutoa mafunzo, kujenga vichanja vya kukaushia dagaa na ununuzi wa boti ya kisasa ya doria. Awamu hii tunanunua boti mbili, mashine ya kusaga mwani na kujenga makaushio mapya,” amesema Kanali Masalamado.
Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Japan kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Kwa upande wake, mwakilishi wa UNDP, Saimon Nkonoki, alisema:“Tumefurahi kuona ushirikiano mkubwa kutoka kwa wakulima. Tunaamini mafunzo haya yakitekelezwa kwa vitendo yataongeza mapato na kuboresha maisha ya jamii. Tutaendeleza ushirikiano huu na wadau wa maendeleo nchini,” alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Rashid Karim Gembe, alitoa pongezi kwa serikali na wafadhili akisema mafunzo hayo yataibua mapinduzi makubwa ya mnyororo wa thamani wa mwani. “Tutahakikisha tunawashika mkono wakulima ili kufanikisha malengo ya zao hili,” alisema.
Wakulima waliohudhuria mafunzo walieleza matumaini makubwa ya kuinua uchumi wao kupitia maarifa mapya.
Aisha Jumbe, mmoja wa washiriki, alisema:“Tunao uelewa mpya kuhusu huduma za kifedha, mahitaji ya soko na utunzaji wa fedha. Hii itasaidia kuboresha bidhaa zetu kama sabuni, dawa na mbolea za mwani. Tunaamini tutalipa zao hili heshima inayostahili,” alisema kwa niaba ya wenzake.
Kwa ujumla, mwani unaendelea kuibuka kama zao la kimkakati litakaloweza kuwakomboa wakulima kiuchumi endapo changamoto zilizopo zitashughulikiwa ipasavyo. Kupitia mafunzo, uboreshaji wa mbinu za kilimo na uongezaji thamani, sekta hii inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa si tu ajira kwa vijana na wanawake, bali pia pato la taifa kupitia soko la kimataifa.


