NEW DELHI, India
TAKWIMU za wanafunzi 13,000 kujiua kila mwaka zimewaibua wataalamu wa afya ya akili nchini India, wakizitaka mamlaka kuamka na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na tatizo hilo.
Kiwango hicho ni kikubwa, kiasi kwamba ni asilimia 7.6 ya vifo vya kujiua nchini India, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Taasisi ya Takwimu za Uhalifu.
Kwa kuwa takwimu hizo ni za mwaka 2022, wataalamu wanaonya kuwa huenda tatizo limeongezeka katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Aidha, tafiti zinaonesha kuwa chanzo kikubwa cha tatizo ni msongo wa mawazo unatokana na ugumu wa mitihani, uhaba wa ajira, pamoja na idadi ndogo ya vituo vya elimu ya saikolojia.
Akizungumzia hilo, mtaalamu wa saikolojia, Anjali Nagpal, amesema bado mfumo wa elimu chini India hauwawezeshi wahitimu kukabiliana na presha ya aidha kufeli mitihani au kukosa ajira.
“Tunawaandaa tu kwa ajili ya mitihani, siyo kwa ajili ya maisha. Elimu ya afya ya akili inapaswa kuwa sehemu ya maisha ya shule. Wanafunzi wanahitaji kupewa nafasi ya kuzungumza na kusikilizwa. Waalimu nao wanahitaji kufundishwa namna ya kusikiliza, siyo tu kufundisha.”
Mwanzoni mwa wiki hii, Waziri wa Elimu wa India, Sukanta Majumdar, akiwa Bungeni aligusia hali ilivyo mbaya juu ya matukio ya wanafunzi kujiua.
Waziri huyo alikiri ukubwa wa tatizo, pia akieleza kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua, ikiwamo kusisitiza elimu ya saikolojia ili kuwawezesha wanafunzi kukabiliana na msongo wa mawazo utokanao na ugumu wa masomo au mitihani.
Wakati huo huo, Maheshwer Peri, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Careers360, anasema inasikitisha kuona mtihani wa siku moja ukitumika kupima uwezo wa mwanafunzi.
“Wengine hushindwa kuhimili presha ya kufeli, hivyo kuchukua uamuzi wa kujiua. Ni jukumu letu sasa kuwawekea mazingira ya kuwalinda,” anasema Peri.
Katika utafiti mwingine wa mwaka 2019 uliofanywa na Chuo Kikuu cha Melbourne cha Australia, asilimia 12 ya wanafunzi walihojiwa na kukiri kuwa waliwahi kupata wazo la kujitosa uhai.
Utafiti huo ulioihusisha pia Taasisi ya Afya ya Akili ya India, uliwafikia na kuwahoji wanafunzi zaidi ya 8,500 kutoka vyuo vikuu 30 vya majimbo tisa.


