9.5 C
New York

IUCN na JET kuwanoa waandishi katika kuandika masuala ya Uchumi wa Buluu

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Mradi wa Bahari Mali, unaotekelezwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), unalenga kuonesha mifano ya vitendo ya uchumi wa buluu endelevu na shirikishi nchini Tanzania kwa kuboresha maisha ya jamii za pwani, kuimarisha ulinzi wa mifumo ya ikolojia ya baharini, na kukuza ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi. Moja ya vipengele muhimu vya mradi huu ni kuongeza uelewa wa umma na kushawishi sera kupitia mawasiliano madhubuti.

Katika kutimiza azma hiyo, IUCN kupitia Mradi wa Bahari Mali, imeandaa mafunzo ya kujenga uwezo na ziara ya mafunzo kwa waandishi wa habari 15 kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET). Mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea waandishi hao ujuzi wa kitaalamu, maarifa na uelewa wa kina kuhusu masuala ya uchumi wa buluu, na hivyo kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wenye ushawishi wa kuchochea mijadala ya umma, kuongeza uhamasishaji na kushiriki katika mchakato wa sera kuhusu uchumi wa buluu.

Ingawa dhana ya uchumi wa buluu inazidi kutambulika katika ajenda ya maendeleo ya Tanzania, bado ni dhana ngumu kueleweka, haitolewi taarifa za kutosha katika vyombo vya habari, na haijawekewa mkazo wa kutosha katika mawasiliano ya kitaifa. Waandishi wa habari wana nafasi muhimu katika kuunda simulizi za umma, kuwahabarisha wananchi na watoa maamuzi kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, changamoto za uhifadhi, na fursa mpya za kiuchumi.

Hata hivyo, uelewa mdogo wa kiufundi kuhusu utekelezaji wa dhana ya uchumi wa buluu, fursa za kiuchumi, maeneo ya kipaumbele, sayansi ya bahari, mifumo ya ikolojia, sera zinazounga mkono sekta hiyo, pamoja na mbinu za uhifadhi, unazuia waandishi kuweza kuripoti kwa ufanisi. Mafunzo haya yamebuniwa ili kuziba pengo hilo kwa kuchanganya mbinu za warsha na ziara za mafunzo kwa vitendo, ili kuwawezesha waandishi hao kuandika taarifa zenye ushahidi na mvuto, zitakazoendana na malengo ya IUCN, Mradi wa Bahari Mali na mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Buluu.


Kukuza uwezo wa kiufundi wa waandishi wa JET kupitia warsha mahususi na mafunzo kwa vitendo, na hivyo kuwapa uelewa wa kina, stadi na nyenzo zitakazowawezesha kuwa mabalozi wa dhati wa uchumi wa buluu nchini Tanzania, sambamba na kuendeleza juhudi za IUCN na Mradi wa Bahari Mali katika uhifadhi wa bahari.

Kupitia ushuhuda wa moja kwa moja na mafanikio ya Mradi wa Bahari Mali, waandishi wa habari wa JET watakuwa katika nafasi nzuri ya kuandika taarifa zenye mvuto, kuchochea mijadala ya kisera, kuelimisha jamii, na kushiriki kikamilifu katika harakati za kulinda na kuendeleza rasilimali za bahari na pwani kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img