KAMPALA, Uganda
ACHANA na vurugu, wizi wa kura na hata ‘figisu’ zingine. Kwa miaka mingi, huenda taswira nyingine kubwa zaidi ya siasa za Afrika ni namna zilivyotawaliwa na vitendo vya rushwa.
Lakini, nje ya hayo, bila shaka si jambo geni kwako kusikia wanasiasa wa Afrika wakihusishwa na imani za kishirikina, wakiamini zina nafasi kubwa katika kuwawezesha kupata nafasi mbalimbali za uongozi.
Kwamba fedha, umaarufu, elimu na hata uzoefu bado havimfanyi mwanasiasa kujipa uhakika wa ushindi bila kujiongeza kwa kutembelea ‘upande wa pili’.
Ni kama anavyokiri Wilson Watira, ambaye ni mwanasiasa wa Uganda anayasema ni kawaida kwa wagombea wa nafasi za uongozi kwenda kwa ‘babu’ kwa lengo la kujisafishia njia ya kuingia madarakani.
Watira anasimulia mpinzani wake wa kisiasa alivyowahi kukataa kumpa mkono walipokutana ana kwa ana.
“Alinitazama tu, kisha akamchukua karatasi na kufunika mkono wake, ndipo akanisalimia,” anasema Watira aliyekuwa akiwania nafasi ya ubunge.
Watira anasema Uganda, licha ya kwamba Dini ya Ukiristo ndiyo yenye wafuasi wengi zaidi, bado imekuwa ikikumbana na ushindani mkali mbele ya imani za kishirikina. Kwa mujibu wake, hata waumini wa Dini hiyo, wengi wao bado hutembelea kwa Siri vilinge vya ‘mababu’ katika kutafuta suluhisho la matatizo yao.
Ukirudi kwa upande wa wanasiasa, kwa sasa ni kawaida kuona waganga wa kienyeji kupitia matangazo yao, wakijinasibu kuwa wana uwezo wa kumwezesha mgombea kupata nafasi ya uongozi anayoitaka.
Mtafiti na mtaalamu wa masuala ya utamaduni, Steven Masiga, analizungumzia hilo akisema: “Waganga wa kieyenyeji kwa sasa wanajipanga kuvuna fedha za wanasiasa. Hata wanasiasa, wanatenga fedha za waganga kwa sababu ndiyo tumaini lao.”
Masiga anatolea mfano tukio la mgombea wa eneo lake, ambaye akipewa sharti (na mganga) la kumchuna ngozi mbuzi bila kumchinja. “Alishinda katika uchaguzi,” anasema. Kama hiyo haitoshi, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, hajawahi kuficha kuwa ni muumini mzuri wa waganga wa kienyeji.
Katika moja ya hotuba zake za mwaka jana, Rais Museveni alisimulia alivyowahi kuchinja kuku mara tatu, kama sehemu ya imani za kishirikina zilizowawezesha kushinda vita iliyomweka madarakani mwaka 1986.
Pia, katika tukio la mwaka 2016, Spika wa Bunge, Rebecca Kadaga, alipigwa picha akiwa anaingia kwa mganga wa kienyeji huko Mashariki mwa Uganda.
Akijibu baada ya kukosolewa vikali, mwanasiasa huyo alisema haoni tatizo kwenda kwa mganga. “Nani hana asili? Nani hana alikotokea? Ile ni asili yangu,” alisema Kadaga. Ukifika katika Mji wa Mbale, mmoja ya waganga wa kienyeji ni Rose Mukite. Naye anakiri kupokea wanasiasa wengi wanaosaka nafasi za uongozi katika chaguzi mbalimbali.
Mukite anasema alianza kazi hiyo mwaka 1980 baada ya kurithishwa. Anasema kama asingekuwa anasaidia, basi angeshapoteza wateja na kuiacha kazi hiyo miaka mingi iliyopita. “Nina wateja wengi. Nimewasaidia wanasiasa wengi, hasa kwenye majanga, ikiwamo kuwaepusha na vifungo vya jela katika kesi zao.
Hata hivyo, Mukite anakiri kuwa aliwahi kufeli katika baadhi ya huduma zake. “Siwezi kusema nimefaulu kila mtihani. Unakuta mwanasiasa anakuja akiwa amechelewa. Ni kama hospitali, siyo kila mgonjwa atapona,” anasema.
Lakini, si Uganda pekee. Mathalan, Sudan Kusini nayo imeelezwa kuwa ni moja ya maeneo ya Afrika, ambayo imani za kishirikina imetamalaki. Achilia mbali Sudan Kusini, Taifa jingine la Ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kenya, nalo limekuwa likitajwa kuwa na changamoto hiyo.
Wakati fulani, wananchi wa Kenya walioandama jijini Nairobi wakiipinga Serikali walisema walikumbana na hali mbaya ya kiafya walipokaribia makazi ya Rais William Ruto jijini Nairobi. Walichoamini ni kwamba hali hiyo ni matokeo ya ‘mizimu’ inayomlinda Rais Ruto na kumwekea kinga ili abaki madarakani.
Kama itakumbukwa, pia waandamanaji hao walikosoa kanisa alilojenga ndani ya Ikulu, wakisema si nyumba ya ibada, bali ni sehemu ya kufanyia ushirikina. Ukiiweka kando Kenya, Zambia nayo iliwahi kuwa na tukio la wanaume wawili kushikiliwa na vyombo vya dola kwa shutuma za kutaka ‘kumroga’ Rais Hakainde Hichilema.
Ikumbukwe, Rais Hichilema naye aliwahi kukwaa skendo ya kumfanyia vitendo vya kishirikina mtangulizi wake, Michael Sata.


