LONDON, England
HARAKATI za usajili wa majira ya kiangazi zinaendelea barani Ulaya, huku macho yakielekezwa zaidi kwa klabu za England, Bundesliga, La Liga, Ligue 1 na Serie A.
Makala haya yanakuchambulia dili 10 zilizotikisa vichwa vya habari kufikia hatua hii ya usajili wa dirisha kubwa.
JOBE BELLINGHAM (SUNDERLAND – DORTMUND)
Kiungo mwenye umri wa miaka 19 na ameigharimu Borussia Dortmund kitita cha Pauni milioni 27.
Bellingham alikuwa sehemu ya kikosi cha Sunderland kilichopanda darajana kurejea Ligi Kuu ya England (EPL).
ESTEVAO WILLAIN (PALMEIRAS – CHELSEA)
Winga mwenye umri wa miaka 18 aliyetua Stamford Bridge kwa ada ya Pauni milioni 29. Estevao ameondoka Brazil akiwa ameifungia Palmeiras jumla ya mabao 26 katika michezo 77.
JEREMIE FRIMPONG (LEVERKUSEN – LIVERPOOL)
Beki wa kulia mwenye umri wa miaka 24. Liverpool wamemng’oa Bayern Leverkusen kwa Pauni milioni 29.
Usajili wake umelenga kuziba pengo la mlinzi aliyetimkia La Liga kujiunga na Re Madrid, Trent Alexander-Arnold. Amesaini miaka mitano Anfield.
MATHYS TEL (BAYERN – TOTTENHAM)
Tottenham wametumia Pauni milioni 30 kumng’oa moja kwa moja Bayern Munich baada ya kuwa naye kwa mkopo. Mshambulia huyo ana umri wa miaka 20 na alifunga mabao matatu katika mechi 20 alizocheza Tottenham. Amesaini mkataba wa miaka sita.
LIAM DELAP (IPSWICH – CHELSEA)
Straika mwenye umri wa miaka 22, ambaye ameigharimu Chelsea kiasi cha Pauni milioni 30 akitokea Ipswich Town. Msimu uliopita, Delap aliyewahi kukipiga Manchester City alifunga mabao 12. Chelsea wamempa mkataba wa miaka sita.
RAYAN CHERKI (LYON – MAN CITY)
Kiungo mshambuliaji aliyetua Etihad kwa Pauni milioni 30. Cherki ana umri wa miaka 21. Ameondoka Lyon akiwa na mabao 29 katika mechi 185.
RAYAN AIT-NOURI (WOLVES – MAN CITY)
Beki wa kushoto mwenye umri wa miaka 24, ambaye usajili wake umeigharimu Manchester City kitita cha Pauni milioni 31. Ait-Nouri aliyeitumikia Wolves kwa misimu mitano, alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Man City majira haya ya kiangazi.
JEAN-CLAIR TODIBO (NICE – WEST HAM)
Beki wa kati aliyekuwa akiwindwa na Manchester United, kabla ya kusajiliwa moja kwa moja na West Ham United kwa Pauni milioni 34. Todibo akiwa kwa mkopo West Ham, alicheza mechi 29. Mlinzi huyo ni raia wa Ufaransa na ana umri wa miaka 25.
JAMIE GITTENS (DORTMUND – CHELSEA)
Winga huyo kutoka Borussia Dortmund aliwahi kupita katika ‘academy’ ya Chelsea na sasa amerejea kwa Pauni milioni 48. Gittens mwenye umri wa miaka 20, amesaini mkataba wa miaka saba kuwatumikia wakali hao wa Stamford Bridge.
DEAN HUINSEN (BOURNEMOUTH – MADRID)
Bournemouth walimsajili kutoka Juventus na sasa beki wa kati huyo amejiunga na Real Madrid kwa Pauni milioni 50. Hiyo ni biashara nzuri kwa Bournemouth kwani wao walimng’oa Juventus kwa ada ndogo tu ya Pauni milioni 12.8.
MOHAMED KUDUS (WEST HAM – TOTTENHAM)
Mshambuliaji mwenye umri wa miaka 24, ambaye Tottenham wamemsajili kwa Pauni milioni 55.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24, amesaini mkataba wa miaka sita kukipiga Kaskazini mwa London.
JOAO PEDRO (BRIGHTON – CHELSEA)
Akiwa na umri wa miaka 23 tu, Pedro ni mshambuliaji anayemudu nafasi za straika au kiungo mshambuliaji (nambie 10). Chelsea wametumia Pauni milioni 55 kukamilisha usajili wake na kumpa mkataba mrefu wa miaka nane.
MARTIN ZUBIMENDI (SOCIEDAD – ARSENAL)
Kiungo mwenye umri wa miaka 26, ambaye Arsenal wametumia Pauni milioni 56 kuinasa saini ya Mhispania huyo. Liverpool walijaribu bila mafanikio kumsajili mwaka jana. Zubimendi ni mshindi wa taji la EURO 2024.
MATHEUS CUNHA (WOLVES – MAN UNITED)
Manchester United wamemsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kwa dau la Pauni milioni 63.
Kwa ada hiyo, Cunha anakuwa mchezaji wa kwanza kuuzwa kwa dau kubwa zaidi katika historia ya Wolves.
FLORIAN WIRTZ (LEVERKUSEN – LIVERPOOL)
Kiungo mshambuliaji mwenye umri wa miaka 22. Liverpool wamekamilisha usajili wake baada ya kuweka mezani kitita cha Pauni milioni 100. Kabla ya Liverpool kuvunja rekodi yao ya usajili wa beki mbaya, Wirtz alikuwa akiwaniwa pia na klabu za Manchester City, Bayern Munich na Real Madrid.


