LAGOS, Nigeria
TUKIO la kikundi cha waasi nchini Nigeria kuvamia moja ya shule na kuteka wanafunzi 315 limechukua sura mpya.
Wanafunzi hao walivamiwa Ijumaa ya wiki iliyopita wakiwa katika mazingira ya Shule yao ya Kikatoliki iliyopo katika Jimbo la Niger.
Sasa, mwendelezo wa taarifa hiyo ni kwamba wanafunzi 50 kati ya wale waliochukuliwa wamefanikiwa kuwatoroka waasi hao.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Umoja wa waumini wa Dini ya Ukiristo, watoto hao wamerejea nyumbani na kuungana na familia zao.
Kwa upande mwingine, Serikali imeeleza kuwa inaendelea na operesheni zinazoongozwa na jeshi ili kuwapata wanafunzi wengine 265 na waalimu wao 12.
Mamlaka pia zimezitaka shule kutokuendelea na masomo kwa muda kutokana na hali mbaya ya usalama katika maeneo mengi.
Ikumbukwe, kabla ya tukio hilo, tayari zilikuwapo taarifa za Jumatatu ya wiki hii, kwamba waasi walivamia shule ya bweni na kuteka wanafunzi 20 katika Jimbo la Kebbi.
Wakati huo huo, watu 38 waliokuwa wametekwa katika tukio la waasi kuvamia kanisa wiki iliyopita mjini Kwara wameripotiwa kuachiwa.
Published:


