Na Mwandishi Wetu, Gazetini
VIONGOZI wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) wa Mkoa wa Dar es Salaam wapatao 180 wamepatiwa mafunzo ya awali ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuwawezesha kuzishauri menejimenti za taasisi zao kuboresha mazingira ya kazi na kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Mafunzo hayo, yaliyohusisha wenyeviti na makatibu wa matawi yote 90 ya TUGHE mkoani humo, yamefanyika katika kikao kazi cha siku mbili kilichofanyika Kibaha, mkoani Pwani, Oktoba 21 na 22, 2025, ambapo viongozi 180 walishiriki.
Miongoni mwa mada zilizowasilishwa na wataalamu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni pamoja na: Dhana ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Uwakilishi na Kamati za Afya na Usalama Mahali pa Kazi, Mfumo wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi na Misingi ya Huduma ya Kwanza Mahali pa Kazi.
Wataalamu wa OSHA, Simon Lwaho na Moteswa Meda, walisisitiza umuhimu wa washiriki kuhamasisha wafanyakazi wenzao kujifunza kanuni bora za usalama na afya kulingana na shughuli zao za kila siku, ili kupata mbinu bora za kujilinda dhidi ya vihatarishi vya ajali na magonjwa kazini.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi hicho, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema viongozi wa TUGHE wana nafasi muhimu katika kushawishi menejimenti za taasisi zao kuboresha mazingira ya kazi kwa ustawi wa wafanyakazi.
“Kupitia kikao kazi hiki tumewaeleza wenzetu wa TUGHE jitihada za Serikali katika kuimarisha afya, usalama na ustawi wa wafanyakazi. Mbali na kuiwezesha OSHA kusimamia taratibu za usalama na afya, masuala haya sasa yamejumuishwa kwenye kanuni za kudumu za utumishi wa umma na kuzingatiwa katika ukaguzi wa CAG na Tume ya Utumishi wa Umma,” alisema Mwenda.
Ameahidi kuwa OSHA itaendelea kushirikiana na TUGHE na vyama vingine vya wafanyakazi kuhakikisha wafanyakazi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu kanuni bora za usalama na afya, zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa usalama na afya njema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Komredi Brendan Maro, aliipongeza OSHA kwa ushirikiano mzuri na mchango mkubwa katika utoaji wa elimu kwa wanachama wao.
“Tunawashukuru sana OSHA kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitupatia, hususan katika kutoa elimu muhimu kwa wanachama wetu ambao ni wafanyakazi,” amesema Komredi Maro.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Norbetha Sanga, Katibu wa TUGHE Tawi la Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa wafanyakazi na waajiri kwani yanachangia kuimarisha usalama, afya na uzalishaji wenye tija katika maeneo ya kazi.Polisi Dar yaonya vurugu wakati wa uchaguzi.


