MADRID, Hispania
MIEZI 14 iliyopita, Trent Alexander-Arnold aliondoka Liverpool akiwa mmoja ya walinzi wa kulia wenye viwango bora Ligi Kuu ya England (EPL) na Ulaya kwa ujumla.
Hata hivyo, msimu wake wa kwanza (2025-26) akiwa Real Madrid haukuwa mzuri. Majeraha yalimfanya azitazame mechi nyingi akiwa nje ya uwanja.
Majeraha makubwa zaidi ni yake ya Septemba, 2025, ambapo alikaa nje ya uwanja kwa wiki saba. Pia, aliumia tena miezi mitatu baadaye na kukosekana kwa wiki nne.
Kwa ufupi, licha ya kusajiliwa kwa Pauni milioni 8.4, beki huyo alimaliza msimu huu akiwa amecheza mechi 21 pekee za Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).
Kwa takwimu za michuano yote, alitumika mara 35, zote akitokea benchi, kati ya mechi 62 walizocheza Madrid msimu wa 2025-26. Nafasi yake alitumika zaidi Dani Carvajal.
Siku chache zijazo, Alexander-Arnold raia wa England, atauanza msimu wake wa pili akiwa Madrid. Safari hii, atakuwa chini ya kocha raia wa Ureno, Jose Mourinho, baada ya kufanya kazi na Xabi Alonso na Alvaro Arbeloa.
Alexander-Arnold amemzungumzia ‘Special One’ akisema ni faraja kwake kufanya kazi na kocha huyo wa zamani wa Chelsea, Manchester United na Tottenham. “Mara zote nimekuwa nikivutiwa naye,” amesema.
“Nimecheza dhidi yake mara nyingi na sasa ni fahari kuwa naye katika timu yake. Sote tunataka na kutamani kujifunza na kuimarika zaidi. Nina uhakika atatufundisha mambo mengi na kutusaidia kutwaa mataji mwaka huu.”
Kwa upande mwingine, changamoto inayomkabili Alexander-Arnold ni ujio wa beki wa kulia raia wa Uholanzi, Denzel Dumfries, ambaye Madrid imemng’oa Inter Milan na kumpa mkataba wa miaka minne.


