MOSCOW, Urusi
SHAMBULIZI la ndege isiyo na rubani linalotajwa kufanywa na Ukraine nchini Urusi limesababisha vifo vya watu 13, akiwamo mtoto.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na mamlaka za Urusi, shambulizi hilo limefanywa katika eneo la Nizhnekamsk na kujeruhi watu wengine 39.
Mamlaka za Urusi zimedai kuwa shambulizi hilo lilichukua saa kadhaa na ni moja ya yale makubwa zaidi kuwahi kufanywa na Ukraine nchini Urusi tangu vita vilipoanza Februari, 2022.
Hata hivyo, bado mamlaka za Ukraine hazijagusia lolote juu ya shambulizi hilo, kwa maana haijakiri kuhusika wala kukanusha.
Nizhnekamsk ni eneo la Urusi lililoko umbali wa kilometa zaidi ya 1,100 kutoka uliko mpaka wa Ukraine. Ni moja ya maeneo yenye viwanda vya mafuta.


