VATICAN CITY, Vatican
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, amehimiza kupatikana kwa amani nchini Sudan katika hotuba yake ya jana Agosti 9, 2026, mjini Vatican.
Kupitia hotuba yake hiyo, Leo aliutaja Mji wa El-Obeid ulioko Kaskazini mwa Jimbo la Kordofan akisema hali ni mbaya kutokana na wakazi wake kukosa chakula, maji na dawa.
Hali ya usalama ni mbaya nchini Sudan kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, msingi wake ukiwa ni kugombea madaraka kati ya wapiganaji wa pande mbili; jeshi la Serikali na kikundi cha Rapid Support Forces (RSF).
“Naendelea kufuatilia na kuumizwa na hali mbaya iliyopo Sudan, hasa katika Mji wa El-Obeid,” amesema Papa Leo.
Wakati huo huo, Papa Leo ameziomba jumuhiya za kimataifa kuingilia kati na kutafuta namna ya kurejesha utulivu katika maeneo mengi ya nchi hiyo.
“Naziomba jumuhiya za kimataifa kuunga mkono jitihada za kumaliza vita. Tuwaombee kwa Mungu wale wanaopitia shida, abadili mioyo ya wale wanaopigana, na kurejesha amani,” amesema.


