5.9 C
New York

Ndoto ya kuunganisha Tanga na Pwani ya Afrika Mashariki mbioni

Published:

*Ujenzi wake wafikia asilimia 74.3

Na Mwandishi Wetu, Gazetini-Tanga

UJENZI wa Daraja la Pangani mkoani Tanga, lenye urefu wa mita 525 pamoja na barabara unganishi na mchepuko zenye jumla ya kilomita 25, umefikia asilimia 74.3 hadi kufikia Septemba 30, 2025.

Kati ya kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa kuta mbili unganishi za daraja (abutments) na nguzo nane za kati (piers), huku zaidi ya Sh bilioni 45.6 zikiwa zimeshalipwa kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama Msama, amesema wakati wa ziara yake ya ukaguzi leo Oktoba 14, 2025, kuwa daraja hilo litakapokamilika litakuwa chachu kubwa ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii katika mkoa huo na maeneo jirani.

“Daraja hili litapunguza muda wa usafiri, kurahisisha biashara, kuongeza mwingiliano wa wananchi, kufungua fursa za utalii, na kuwa kiungo muhimu kati ya bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa — hivyo kuchochea zaidi uchumi wa buluu,” amesema Mhandisi Msama.

Daraja hilo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kufungua na kuimarisha miundombinu ya usafiri katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki unaoanzia Malindi – Mombasa – Lunga Lunga/Horohoro – Tanga – Pangani – Bagamoyo (Makurunge) wenye urefu wa kilomita 454.

Kwa mujibu wa Mhandisi Msama, ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani yenye urefu wa kilomita 50 — ambayo ni sehemu ya kwanza ya mradi huo — unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na unatekelezwa na kampuni ya CHICO kutoka China, ukiwa umefikia asilimia 75.

Sehemu ya pili ya mradi ni ujenzi wa Daraja la Pangani na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 25.6, unaofadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Sehemu ya tatu ni barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange yenye urefu wa kilomita 95.2, ambayo imefikia asilimia 53 ya utekelezaji na inagharimu Sh bilioni 94.54.

Aidha, barabara hiyo inatarajiwa kuchochea ongezeko la uzalishaji wa mazao ya kilimo hususan mihogo, nazi na mwani, na hivyo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda kwenye masoko mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Tanga.

Vilevile, TANROADS Mkoa wa Tanga inaendelea kutekeleza miradi mitatu ya dharura iliyosababishwa na mvua za El Niño na Kimbunga Hidaya kwa gharama ya Sh bilioni 11.27.

Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa Daraja la Msangazi lenye urefu wa mita 30 katika barabara ya Amani – Muheza kwa Sh bilioni 4, daraja la boksi la Bwiko lenye urefu wa mita 16.5 na barabara unganishi za mita 630 litakalogharimu Sh bilioni 3, na Daraja la Sagasa lenye urefu wa mita 39 katika barabara ya Kwaluguru – Kiberashi litakalogharimu Sh bilioni 4.1.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img