YERUSALEMU, Israel
Wapenzi wa Israel walioitwa ‘Romeo na Juliet’ wameungana tena baada ya zaidi ya miaka miwili tangu kutenganishwa na mashambulizi ya Hamas.
Noa Argamani, aliyekuwa mateka aliyekolewa Juni 2024 katika operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza, ameonekana tena akiwa ameungana na mpenzi wake, Avinatan Or, ikiwa ni zaidi ya miaka miwili tangu walipotenganishwa kwa nguvu na wapiganaji wa Hamas Oktoba 7, 2023.
Picha zenye hisia kali zinaonyesha wawili hao wakikumbatiana kwa furaha kubwa, ishara ya ushindi wa upendo juu ya maumivu na uovu. Noa, mwenye umri wa miaka 27, alitekwa akiwa na Avinatan (32), katika tamasha la muziki la Nova, tukio lililokuwa mfano wa mateso ya siku hiyo.
Avinatan, ambaye kwa muda mrefu utambulisho wake ulifichwa kwa sababu za kiusalama, sasa amefahamika kuwa ni askari wa kikosi maalumu cha Sayeret Matkal, kinachojulikana kama “Israeli SAS”, kikosi mashuhuri kwa oparesheni za ujasusi na uokoaji wa mateka.
Wakiwa hospitalini, Avinatan alionekana akimkumbatia Noa kwa mapenzi makubwa na baadaye kuungana na wazazi wake, Ditza na Yaron, huku akiwaonyesha ishara ya moyo kwa wafuasi waliokuwa wakishangilia nje.
Noa, ambaye alihutubia maafisa wa juu wa Marekani wiki chache kabla ya kuokolewa kwake, aliapa kutokata tamaa hadi pale Avinatan atakapokuwa huru -kauli ambayo sasa imekuwa ishara ya ushindi wa matumaini na ujasiri.


