Na Malima Lubasha, Gazetini-Serengeti
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameipongeza Taasisi ya Nyansaho Foundation kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jamii, ikiwemo misaada na huduma mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 4 zilizotolewa katika mkoa huo.
Kanali Mtambi alitoa pongezi hizo wakati wa hafla ya kukabidhi mabasi matatu yaliyotolewa na taasisi hiyo kwa shule za sekondari za Natta, Ngoreme na Mchochwe wilayani Serengeti. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni katika ofisi za Nyansaho Foundation zilizopo mjini Mugumu.
Mabasi hayo yenye thamani ya jumla ya Sh milioni 372 yametolewa kufuatia ahadi iliyotolewa na Muasisi wa taasisi hiyo, Dk. Rhimo Nyansaho, kwa shule hizo.
“Shilingi bilioni 4 zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji na mahitaji maalum. Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi, na msaada huu wa mabasi utarahisisha usafiri wa wanafunzi na walimu katika shughuli za kielimu,” alisema Kanali Mtambi.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo imekuwa mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali katika kuchochea maendeleo endelevu.
“Fedha hizo siyo kidogo. Zimechangia miradi mingi ya maendeleo wilayani Serengeti na katika mkoa wa Mara kwa jumla. Natoa wito kwa taasisi nyingine binafsi kuiga mfano wa Nyansaho Foundation katika kusaidia jamii,” alisisitiza Mtambi.
Kwa upande wake, Dk. Rhimo Nyansaho alisema pamoja na msaada huo wa magari, taasisi yake imeendelea kuchangia vifaa vya kielimu na miradi mingine ya kijamii katika shule hizo.
“Kila basi lina thamani ya Sh milioni 124, na tumehakikisha limekamilika kwa ubora wa juu. Tunatoa wito mabasi haya yatunzwe vizuri ili yaweze kudumu na kuwasaidia wanafunzi kwa muda mrefu,” alisema Dk. Nyansaho.


