WASHINGTON DC, Marekani
DAWA ambayo ni kinga dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi sasa itauzwa kwa Dola 40 (Shilingi 99,061 za Tanzania), ikiwa ni punguzo la asilimia 0.1 ya bei ya awali.
Katika mpango huo, kinga hiyo ya sindano inayofahamika kwa jina la Lenacapavir itazifikia nchi masikini zaidi ya 100 miaka miwili ijayo.
Kwa mujibu wa wanasayansi, dawa hiyo ina uwezo mkubwa wa kuzuia virusi vya Ukimwi kujizalisha zaidi ndani ya mwili, hivyo kusaidia kupunguza maambukizi mapya.
Kinga hiyo ni kwa njia ya sindano, ambapo mtu atalazimika kuchoma mara mbili kwa mwaka (kila baada ya miezi sita) ili kujikinga na Ukimwi.
Mpango wa punguzo la bei kwa mataifa yanayokuwa kiuchumi umekuja baada ya makubaliano kati ya Taasisi ya Clinton Health Access Initiative kwa kushirikiana na Mfuko wa Gates, sambamba na washirika wengine, ikiwamo Taasisi ya Tafiti ya Afrika Kusini (Wits RHI).
“Kwa mataifa ya kipato cha chini na kati, uwezo wa kupata kinga ya Ukimwi siyo suala la anasa, ni la lazima,” amesema Profesa Saiqa Mullick kutoka Wits RHI.
Baada ya majaribio kadhaa, Lenacapavir imeonekana kuwa na matokeo chanya na hata kuthibitishwa na Shirika la Afya ya Umoja wa Mataifa (WHO) kuwa kinga ya Ukimwi.
Published:


