LONDON, Uingereza
TUKUTANE Januari. Zipo dili nyingi zilizokwama wakati wa usajili wa dirisha kubwa lililofungwa hivi karibuni na sasa zinasubiri Januari.
Je, ni dili zipi zilizoshindwa kukamilishwa hadi usajili wa kiangazi ulipofungwa Agosti 31, mwaka huu? Makala haya yanakuchambulia.
MARC GUEHI (PALACE – LIVERPOOL)
Liverpool ilishakubaliana na Crystal Palace na ilionekana wazi kuwa beki wa kati huyo angetimkia Anfield.
Baada ya Liverpool kuweka mezani kiasi cha Pauni milioni 35, ilifika hatua ya video kuvuja zikimuonesha Guehi akiwaaga wachezaji wenzake wa Palace.
Hata hivyo, dili liliota mbawa dakika za mwisho kuelekea kufungwa kwa usajili. Taarifa zinaeleza kuwa Palace watakuwa tayari kukaa mezani na Liverpool ifikapo Januari, mwakani.
ADEMOLA LOOKMAN (ATALANTA – BAYERN)
Bayern Munich ilikuwa kwenye mawindo ya mshambuliaji huyo kwa kipindi kirefu cha usajili wa majira haya ya kiangazi. Klabu hizo zilikaa mezani lakini Atalanta iligoma dakika za mwisho kumwachia nyota huyo.
Ni baada ya Bayern kumtaka kwa mkopo, wakati Atalanta ikishinikiza ufanyike usajili wa moja kwa moja. Taarifa zilizopo zinafichua kuwa huenda nyota huyo akajiunga na Juventus au Napoli kupitia dirisha dogo la Januari.
JAVI GALAN (ATLETICO – FOREST)
Kila kitu kilishakamilika juu ya dau la mchezaji huyo na alikaribia kabisa kutua Ligi Kuu ya England akitokea La Liga. Beki wa pembeni huyo mwenye umri wa miaka 30, alishakubali mkataba wa miaka mitatu na Forest.
Lakini, dili lilikwama dakika za mwisho na hatimaye Galan kubaki Atletico Madrid. Bado nyota huyo wa kimataifa wa Hispania ameonesha nia ya kuondoka Atletico na huenda hilo likatokea Januari.
VICTOR BONIFACE (LEVERKUSEN – MILAN)
Mshambuliaji huyo alikaribia kujiunga na AC Milan kwa mkataba wa mkopo, ambao ungeiruhusu klau hiyo ya Serie A kumsajili moja kwa moja hapo baadaye.
Kilichokwamisha biashara ni vipimo vya afya, ambapo Milan walibaini kuwa Boniface raia wa Nigeria ana historia ya majeraha sugu.
Lakini, Boniface alizungumzia hilo akisema Milan walitazama majeraha ya zamani na si hali yake ya sasa. “Niliumia goti mara mbili, lakini ni majeraha ya zamani,” alisema.
Je, Bayern inasubiri Januari ili kumrudia nyota huyo aliyefunga mabao 32 na kutoa ‘asisti’ 12 tangu alipotua Leverkusen mwaka 2023?
NICO WILLIAMS (BILBAO – BARCELONA)
Mwanzoni kabisa mwa usajili wa dirisha kubwa, Barca walikaa mezani na wakala wa Williams na kufikia hatua nzuri ya kufanya biashara.
Ni wakati huo pia, Bayern Munich nayo ilikuwa ikijaribu kumshawishi winga huyo mwenye umri wa miaka 22. Hata hivyo, katika dakika za mwisho za usajili, Williams raia wa Hispania aliamua kusaini mkataba mpya wa miaka 10 na Athletic Bilbao.
Williams aliamua kubaki na kaka yake, Inaki, ambaye pia anakipiga Bilbao tangu alipoibuliwa na ‘academy’ ya klabu hiyo. Endapo Barca itaamua kumrudia Januari, basi italazimika kuweka mezani si chini ya euro milioni 90. Je, itafanya hivyo?
EMI MARTINEZ (VILLA – MAN UNITED)
Kipa huyo wa Aston Villa alishafanya mazungumzo na kocha wa Man United, Ruben Amorim, tangu Juni, mwaka huu. Mambo yaligeuka ghafla na hatimaye Martinez kuendelea kulilinda lango la Villa.
Kwa upande wao, mabosi wa Man United waliziba pengo hilo kwa kumsajili kipa raia wa Ubelgiji, Senne Lammens. Kwa usajili wa Januari, Man United kumrudia Martinez itategemea na kiwango cha makipa waliopo, akiwamo huyo aliyetokea Royal Antwerp ya Ubelgiji.
Published:


