9.5 C
New York

Chupa za kioo changamoto kwa mazingira, TBL, PETPRO waja na suluhisho

Published:

Na Jonathan Benedict, Gazetini

Kila mwaka, maelfu ya tani za chupa za kioo hutupwa nchini Tanzania baada ya matumizi. Tafiti za mazingira zinaonyesha kuwa chini ya asilimia 10 ya taka hizo ndizo hukusanywa na kuchakatwa upya, huku zaidi ya asilimia 90 zikibaki kutupwa dampo, mitaani na katika vyanzo vya maji.

Chupa hizo huchukua mamia ya miaka kuyeyuka, na mara nyingi husababisha uchafuzi wa mazingira, kuharibu mandhari na hata kuongeza hatari za kiafya kutokana na vipande vinavyoweza kujeruhi.

Ni changamoto ambayo pia huathiri miji na vijiji, ambapo taka za kioo hujazana katika maeneo ya wazi, zikikosa mfumo rasmi wa ukusanyaji na uchakataji.

Hali hii imekuwa ikionekana kama pengo kubwa katika jitihada za kitaifa za kulinda mazingira na kusimamia taka kwa njia endelevu.

Sasa, Kampuni ya Tanzania Breweries Plc (TBL) kwa kushirikiana na PETPRO zimeweka historia kwa kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuzindua mfumo wa kwanza wa kitaifa wa ukusanyaji na urejelezaji wa chupa za kioo baada ya matumizi. Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Makao Makuu ya TBL, Ilala, Dar es Salaam.

Mpango huu unalenga kupunguza kwa kiasi kikubwa chupa za glasi zinazotupwa dampo, kuongeza viwango vya uchakataji na kuzibadili taka kuwa malighafi zenye thamani.

Hatua hii inatarajiwa kuchangia katika kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi, kulinda maliasili na kuimarisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Taifa sambamba na Mkakati wa Maendeleo Endelevu wa TBL 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, amesema: “Ushirikiano huu na PETPRO ni mfano wa kuigwa kwa wazalishaji. Unachochea uboreshaji wa uzalishaji, utunzaji wa mazingira na ukuaji wa uchumi. Tunatarajia mpango huu kuwa jukwaa la kuimarisha uwajibikaji wa wazalishaji nakutumia uwezo wa pamoja kufanikisha matokeo makubwa zaidi.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PETPRO, Nicholaus Jackson, amesema:“Kupitia ushirikiano huu, tunaweka mfano mpya wa kuchakata taka za chupa za glasi nchini. Tutaunganisha uzoefu wetu ili kukusanya, kuchakata na kuendeleza mbinu zitakazoboresha mazingira na kutoa fursa za kiuchumi kwa Watanzania.”

Mbali na manufaa ya kimazingira, mradi huu unatarajiwa kutoa ajira na kipato kwa maelfu ya wakusanyaji taka, wachakataji na wazalishaji katika jamii mbalimbali. Kupitia mahitaji ya chupa zilizochakatwa, mfumo huu utawapa Watanzania wengi kipato cha uhakika huku ukichangia kupunguza umasikini.

PETPRO itatoa utaalamu wa uchakataji na usafirishaji, huku TBL ikitumia mtandao wake mpana wa usambazaji kuongeza ufanisi wa urejelezaji. Ushirikiano huu unawekwa kama mfano wa kuigwa na sekta nyingine, ukionyesha kuwa biashara na uwajibikaji wa mazingira vinaweza kwenda sambamba.

Makubaliano haya yanaweka TBL na PETPRO katika nafasi ya kuwa waanzilishi wa mabadiliko ya kijani nchini, wakiahidi kushirikiana na serikali, mamlaka za mitaa na wadau wengine kuboresha na kupanua mfumo wa kitaifa wa urejelezaji chupa za kioo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img