MADRID, Hispania
MSIMU ujao wa La Liga unaotarajiwa kuanza Agosti 15, mwaka huu, ni wa kwanza kwa Xabi Alonso akiwa kocha wa Real Madrid na kibarua kikubwa alichonacho ni kuivua Barcelona taji hilo na kulipeleka Santiago Bernabeu.
Kukosa ubingwa wa La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya kuligharimu kibarua cha kocha raia wa Italia, Carlo Ancelotti, na nafasi yake kuchukuliwa na Alonso aliyetokea Bayern Leverkusen.
ALONSO KUANZA NA ESPANYOL
Msimu mpya utafunguliwa kwa mchezo kati ya Girona na Rayo Vallecano. Girona ilimaliza msimu uliopita ikiwa imenurika kushuka, wakati Vallecano ilishika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa La Liga.
Alonso na vijana wake wa Bernabeu watashuka dimbani Agosti 19 kuivaa Espanyol, siku tatu tu baada ya Barcelona kutupa karata yao ya kwanza kwa kuikabili Real Mallorca.
USAJILI MADRID, BARCA
Kanuni ya nidhamu ya matumizi ya fedha imeibana mbavu Barca, kiasi kwamba usajili wake pekee mkubwa kwa kipindi hiki ni Marcus Rashford aliyetua kwa mkopo akitokea Manchester United.
Madrid, kwa upande wao, wamekimbilia kuimarisha safu ya ulinzi kwa kumchukua Trent Alexander-Arnold kutoka Liverpool, Alvaro Carreras (Benfica) na Dean Huijsen (Bournemouth).
ALONSO NA VITA YA EL CLASSICO
Huu ni mtihani mkubwa kwa Alonso msimu ujao. Madrid ilipoteza mechi zote ilizokutana na Barca msimu uliopita. Ni pamoja na ile iliyopeleka ubingwa wa La Liga kwa wapinzani wao hao.
Mechi hiyo ya Mei 11, mwaka huu, ilimalizika kwa Barca kushinda mabao 4-3, matokeo yaliyofifisha matumaini ya Ancelotti kubaki kwenye benchi la ufundi la Madrid
Kabla ya hiyo, kuna mechi ya Oktoba 26, mwaka jana, iliyomalizika kwa Madrid kutandikwa mabao 4-0. Hiyo ilikuwa ni El Classico ya kwanza msimu uliopita.
Pia, kuna ile fainali ya Super Cup (Januari, mwaka huu), ambapo Madrid walifungwa mabao 5-2. Aprili, Madrid pia walibamizwa mabao 3-2 katika fainali ya Copa Del Rey.
ATLETICO NAO WAMEJIPANGA
Wakati fulani wa msimu uliopita, Atletico Madrid ya kocha Diego Simeone ilikuwa na kasi nzuri ya kushinda mechi 15 mfululizo. ilimaliza mbio za ubingwa ikiwa imezidiwa pointi 14 na Barca.
Atletico haikufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu, ambapo ilishia hatua ya makundi, ikiwamo kuchapwa mabao 4-0 na PSG.
Simeone ameimarisha kikosi kwa kumsajili moja kwa moja beki wake wa mkopo kutoka Barca, Clement Lenglet, pia akimnasa mshambuliaji Thiago Almada alikuwa Lyon kwa mkopo akitokea Botafogo ya Brazil.
Almada (24), anakutana na Julian Alvarez, Antoine Griezman na mtoto wa kocha Simeone, Giuliano Simeone, na kuifanya safu ya ushambuliaji ya Atletico kuwa na makali ya kutosha msimu ujao.
Published:


