8.4 C
New York

Rasheedat Ajibade: Staa Nigeria anayeitoa udenda PSG

Published:

PARIS, Ufaransa
KWA misimu minne mfululizo, Rasheedat Ajibade amekuwa mchezaji muhimu katika safu ya ushambuliaji ya Atletico Madrid na sasa PSG wanajaribu kuinasa saini ya Mnigeria huyo majira haya ya kiangazi.
Rasheedat Ajibade ni mchezaji tegemeo kwa timu ya soka ya wanawake ya Nigeria ‘Super Falcons’ na alikuwa nahodha wakati kikosi hicho kilipotwaa ubingwa wa michuano ya mwaka jana ya WAFCON.
Katika mashindano hayo aliiongoza Super Falcons kutwaa taji lao la 10 akiwa Mchezaji Bora wa mashindano hayo baada ya kuchangia mabao matatu.
Haikuwa mara yake ya kwanza. Ajibade mwenye umri wa miaka 25 alikuwa pia sehemu ya kikosi kilichobeba ubingwa wa WAFCON mwaka 2018 na kushiriki Kombe la Dunia (2023) na michuano ya Olimpiki (2024).
Kwa sasa, PSG wako mstari wa mbele wakihitaji saini yake baada ya nyota huyo kuondoka Atletico Madrid aliyojiunga nayo mwaka 2021 akitokea Avaldsnes ya Norway .
Katika mechi zake 137, amefunga jumla ya mabao 41 na kuiwekezesha klabu hiyo ya mjini Madrid kutwaa mataji matatu.
Kwa upande mwingine, safari ya maisha ya soka ya Ajibade ilianzia mjini Lagos akiwa na klabu ya FC Robo.
PSG, kwa upande wao, licha ya kutawala soka la wanaume nchini Ufaransa, bado haina mafanikio makubwa kwa upande wa timu yao ya wanawake.
Kutokana na utawala wa Lyon katika eneo hilo la soka la wanawake, mabosi wa PSG wanaamini usajili wa Ajibade utakiimarisha zaidi kikosi chao kuelekea msimu ujao.
Lakini, ingawa tetesi zinaendelea kushika kasi katika vyombo vya habari vya Ufaransa na Hispania, PSG hawajapeleka ofa kwa mchezaji huyo.
Wakati huu tetesi zikiendelea, Ajibade ameonekana akifanya mazoezi na waajiri wake wa zamani, Atletico Madrid.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img