8.4 C
New York

Victor Gyokeres kuibeba Arsenal msimu ujao?

Published:

LONDON, England

KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, aliingia sokoni majira haya ya kiangazi akihitaji straika. Msako wake umeinasa saini ya mshambuliaji wa kimataifa wa Sweden, Viktor Gyokeres, ambaye ametua Emirates akitokea Sporting Lisbon ya Ureno.

Gyokeres anakuwa mchezaji mwingine kusajiliwa na Washika Bunduki baada ya Arteta kuwanasa Martin Zubimendi, Christian Norgaard, Kepa Arrizabalaga na Noni Madueke.

Kwa usajili wake ulioigharimu Arsenal kitita cha Pauni milioni 64, sasa Washika Bunduki hao wa London wameeshatumia Pauni milioni 210 kwenye soko la usajili majira haya ya kiangazi.

Matumizi makubwa hayo yamelenga kumaliza ukame wa mataji, ambapo Arsenal imeambulia patupu tangu ilipobeba Kombe la FA mwaka 2020. Klabu hiyo haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu tangu mwaka 2004, licha ya kushika nafasi ya pili kwa misimu miwili mfululizo ya hivi karibuni.

ALIWAHI KUFELI EPL

Baada ya kushindwa kujihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha Brighton, Gyokeres alitimkia kwa mkopo Coventry mwaka 2021.

Akiwa huko, pia mambo hayakwenda vizuri katika msimu wake wa kwanza. Aliishia kufunga mabao matatu pekee katika mechi 19 za Ligi Daraja la Kwanza (Championship).

Misimu miwili baadaye (2021-22 na 2022-23), ndipo Gyokeres alipokunjua makucha yake na kufunga jumla ya mabao 38 katika mechi 91 na hapo Sporting Lisbon ikamsajili kwa ada ya Pauni milioni 21.

MKALI WA MABAO, ‘ASIST’

Gyokeres (27), amejiunga na Washika Bunduki hao wa London akiwa mmoja ya wafungaji bora kuwahi kutokea katika historia ya soka la Ureno.

Hadi anafungasha virago vyake na kuondoka Sporting Lisbon, alishaifungia timu hiyo jumla ya mabao 97, pia akichangia ‘asist’ 26 katika michezo 102.

Ikumbukwe, nyota huyo alimaliza msimu uliopita akiwa ndiye kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Ureno.

Kama hiyo haitoshi, aliingia kambani mara tisa katika majukumu ya timu yake ya taifa ya Sweden.

Hivyo, Gyokeres alikuwa ndiye mchezaji mwenye mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu 10 bora barani Ulaya. Kati ya 39, mabao 12 aliyafunga kwa mikwaju ya penalti.

Kwa kwa miaka 20 ya hivi karibuni, anaungana na Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Robert Lewandowsk na Luis Suarez katika orodha ya wachezaji pekee waliofikisha mabao 39 ndani ya msimu mmoja.

KIBOKO YA SALAH, HAALAND?

Wakati huo huo, Gyokeres ni miongoni mwa washambuliaji wanaobebwa na uwezo wao mkubwa wa kupiga mashuti ya mbali.

Wastani wake wa mashuti ni 4.5 katika kila mchezo, akiwaacha mbali washambuliaji wa Arsenal, Gabriel Jesus (3) na Kai Havertz (2.6).

Ana wastani mzuri wa asilimia 27. 3 ya mashuti yanayozaa mabao. Takwimu zinaonesha kuwa amewazidi na kuwaacha mbali washambuliaji wengi wa Ligi Kuu ya England, wakiwamo mastaa Mohamed Salah (21.1%), Erling Haaland (21.6%) na Alexander Isak (26.4%).

KIVULI CHA NUNEZ KUMFUNIKA?

Gyokeres amejiunga na Arsenal akiwa na historia nzuri ya kile kilichomkuta Darwin Nunez, ambaye naye alitua England akiwa mmoja ya washambuliaji wa kiwango cha juu kutoka Ligi Kuu ya Ureno.

Nunez alisajiiwa na Liverpool baada ya kuwika akiwa na Benfica, ambayo aliifungia mabao 26 katika michezo 28 ya msimu wa 2021-22.

Hata hivyo, nyota huyo ameshindwa kutamba EPL akiwa na ‘uzi’ wa klabu hiyo ya mjini Merseyside.

Je, Gyokeres ataangukia kwenye shimo hilo, au atafuata nyayo za Bruno Fernandes (Manchester United), Ruben Dias (Manchester City) na Evanilson (Bournemouth), ambao wameendeleza makali waliyotoka nayo Ligi Kuu ya Ureno.

SALIBA ANASEMAJE KUHUSU GYOKERES?

Beki wa kati wa Arsenal, William Saliba, aliwahi kukutana mara kadhaa na Gyokeres katika mechi dhidi ya Sporting Lisbon. Je, anamzungumziaje straika huyo?

“Tunajua alivyo mchezaji mzuri, ni tishio unapokutana naye. Kwa kweli nimefurahi kuwa naye kikosini na nina uhakika atatusaidia kushinda mechi na kutwaa mataji,” alisema.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img