WASHINGTON DC, Marekani
JUMATANO ya wiki hii, Rais wa Marekani, Donald Trump, alifungua Mkutano wa siku tatu na viongozi wa nchi tano za Afrika mjini Washington DC. Wageni wa Trump katika Mkutano huo ni marais wa Gabon, Guinea-Bissau, Liberia, Mauritania na Senegal.
Kwa wajuzi wa masuala ya siasa, Mkutano huo haukuwa na taswira ya misaada kwa Afrika, bali namna Marekani inavyoweza kunufaika. Katika Mkutano huo, Rais wa Mauritania, Mohamed Ould Ghazouani, alikuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kuzungumza.
Katika hotuba yake, Ghazouani alimpongeza Rais Trump kwa namna alivyojitosa katika matatizo ya Afrika, akigusia Ikulu ya Marekani ilivyosimamia mazungumzo ya amani kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na majirani zao, Rwanda. Ilipofika zamu ya Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, alisifia uwezo mzuri wa Trump katika mchezo wa gofu.

Faye alimualika Rais Trump kujenga uwanja wa mchezo huo nchini Senegal, jambo ambalo lilionekana kumfurahisha mwenyeji wake huyo. Aidha, marais wa Afrika walitumia Mkutano huo kumtangazia Rais Trump rasilimali zilizopo katika mataifa yao, ikiwa ni fursa kwake na wawekezaji wa Marekani.
Kwa upande wake, Faye wa Senegal alieleza nia yake ya kuifanya Dakar kuwa ‘Mji wa Kiteknolojia’ na kuwaalika wawekezaji wa Marekani katika mpango huo. Rais wa Gabon, Brice Clotaire Oligui Nguema, alisema Taifa lake lina utajiri wa madini, pia akiitahadharisha Marekani kuwa mataifa mengine yatawahi endapo haitachangamkia fursa hiyo.
Kwa mtazamo wake, Balozi wa zamani wa Senegal nchini Marekani, Babacar Diagne, Mkutano huo umelenga kurejesha uhusiano mzuri kati ya Marekani na Bara la Afrika. Kama itakumbukwa, baada tu ya Rais Trump kurudi madarakani Januari, mwaka huu, alitangaza Marekani kusitisha misaada yake kwa Afrika.
Kwa mujibu wa Trump wakati huo, misaada hiyo ilikuwa ni hasara kwa Marekani na isiyoendana na sera ya Taifa hilo ya ‘masilahi yetu kwanza’. Lakini, mwanadiplomasia Diagne anaona uhusiano wa sasa kati ya Marekani na Afrika hautakuwa wa misaada tu, bali biashara inayolinufaisha Taifa hilo kubwa katika nyanja ya uchumi.
“Ni biashara kwa asilimia 100. Kama unataka kuwa upande wake, basi ukubaliane na matakwa yake. Nje ya hapo, basi usitegemee chochote,” anasema Diagne. Katika hilo, inaelezwa pia Marekani itanufaika kwa kiasi kikubwa na madini kutokana na ‘biashara’ ya kusimamia mazungumzo ya amani kati ya DRC na Rwanda.
Naye kwa upande wake, Nicaise Mouloumbi, ambaye ni Mkuu wa Taasisi ya kiraia nchini Gabon, amesema Marekani imeutazama Mkutano huo kwa jicho la ushindani dhidi ya wapinzani wake kiuchumi, Urusi na China.
Mouloumbi anasema Marekani inaona namna wapinzani wake hao wanavyonufaika na rasilimali za mataifa hayo.
“Mataifa yote hayo (yaliyoalikwa na Trump) yana madini muhimu; dhahabu, mafuta, gesi na zircon,” anasema Mouloumbi. Ifahamike, Gabon inamiliki takribani robo ya madini yote ya manganese duniani na imekuwa ikiipatia China asilimia 22 ya madini hayo.
Wakati huo huo, Marekani inazihitaji Mauritania na Senegal, si tu kutokana na rasilimali, bali pia suala la uhamiaji haramu. Kivipi? Kwa mujibu wa Ousmane Sene, ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Utafiti cha Afrika Magharibi (WARC), maelfu ya vijana wanatoka katika mataifa hayo na kuingia Marekani ni suala nyeti kwa Rais Trump.
“Tusisahau kwamba kati ya 2023 na 2025, si chini ya vijana wa 20,000 wa Mauritania na mamia ya wenzao wa Senegal walikimbilia Marekani kupitia Nicaragua,” anasema Sene. “Nchi zote hizi ni kitovu cha uhamiaji haramu na hili ni suala nyeti mno katika sera ya uhamiaji ya utawala wa Trump.”
Vilevile, wapo wanaoamini kuwa Rais Trump kupitia Mkutano huo, alijaribu kuishawishi Mauritania kurejesha uhusiano wake wa kidiplomasia na Israel. Ifahamike kuwa Marekani ni mshirika mkubwa wa Israel ambaye Mauritania alikatisha uhusiano naye baada ya kutoridhishwa na ‘ubabe’ wake dhidi ya Wapalestina huko Gaza.


