11.6 C
New York

Musk, Trump; nini hatima vita ya fedha, mamlaka?

Published:

NA HASSAN DAUDI
HATUA ya bilionea wa teknolojia, Elon Musk, kuanzisha Chama cha siasa cha ‘America Party’ mwishoni mwa wiki hii kimekoleza uhusiano wake mbaya na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Kwa miezi ya hivi karibuni, Musk, ambaye ndiye mmiliki wa mtandao wa kijamii wa ‘X’ (zamani Twitter), amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais Trump na Chama chake, Republican.
Hata uamuzi wa Musk kuja na America Party ulitanguliwa na kitendo cha Rais Trump kusaini mswada ambao tajiri huyo alishaonya kuwa unachochea matumizi makubwa ya Serikali yanayoweza ‘kuifilisi’ Marekani.
Kwa mujibu wa Musk, muswada huo wenye kurasa zaidi ya 1000 utalifanya deni la Taifa kuongezeka mara dufu, kutoka Dola trilioni 2 hadi Dola trilioni 2.5.
“Mbunge yeyote ambaye kampeni zake zilisisitiza Serikali kubana matumizi, halafu akaunga mkono muswada huu, basi anapaswa kuona aibu,” alisema Musk.
URAFIKI WAO
Kabla ya uadui wao wa sasa, Musk na Rais Trump walikuwa marafiki wakubwa miezi kadhaa iliyopita.
Kuthibitisha hilo, Musk alitumia kiasi kikubwa cha fedha (Dola milioni 288) katika kampeni za Trump kurudi madarakani mwaka jana.
Trump alipoingia Ikuku, alimteua Musk kuwa mshauri wake kupitia Idara mpya iliyoundwa ya ‘DOGE’.
Akiwa na Idara hiyo, bilionea huyo alisisitiza kubana matumizi ya Serikali, hatua iliyoondosha ajira za watumishi wengi.
Kutokana na nguvu kubwa ya ushawishi, Musk, kwa mujibu wa wanasiasa wa upinzani, ndiye aliyekuwa akiiingoza Serikali.
Licha ya kukosolewa huko, Trump na Musk waliendelea kuwa na ukaribu mkubwa, kila mmoja akimtaja mwenzake kuwa ni kiongozi bora. “Nampenda Rais, nataka niseme hilo bila kuficha,” alisema Musk akimzungumzia Trump.
UGOMVI ULIANZIA HAPA
Aprili, mwaka huu, Musk alitangaza kuwa atakuwa akitumia muda mchache katika majukumu ya Idara ya DOGE.
Lakini, haikushangaza. Kabla ya hapo, tayari zilikuwepo taarifa kuwa haelewani na baadhi ya watu wa karibu wa Trump.
Mei, mwaka huu, Musk alijitokeza tena, safari hii akilikosoa Bunge. Alipinga mswada aliodai umepuuza kazi kubwa iliyofanywa na Idara yake ya DOGE katika kubana matumizi ya Serikali.
“Nilishangaa kuona muswada unaokithirisha matumizi, ambao unaongeza deni na kupuuza kazi kubwa iliyofanywa na DOGE,” alisema Musk katika mahojiano yake na kituo cha runinga cha CBS.
Kwa upande wake, Trump alimjibu kupitia mitandao ya kijamii akisema Musk amegomea muswada huo kwa kuwa unaondosha ruzuku aliyokuwa akipata kupitia kampuni yake ya magari ya Tesla.
HISTORIA INAJIRUDIA?
Kwa wafuatiliaji wa siasa za Marekani, hii si mara ya kwanza kwa Musk na Trump kuwa ‘chui na paka’. Ilianzia wapi? Endelea.
Siku chache tu baada ya kununua mtandao wa Twitter, Musk alimvaa Trump. Hiyo ilikuwa mwaka 2022.
Katika moja ya ‘post’ zake za Julai, mwaka huo, Musk aliandika: “Trump ni mzee, kiasi kwamba si tu urais, hawezi kuwa kiongozi wa kitu chochote.”
Ni wakati huo, Musk alikuwa akimuunga mkono mpinzani mkubwa wa Trump ndani ya Chama cha Republican, Ron DeSantis.
Kama hiyo haitoshi, Musk alimpa DeSantis nafasi ya kurusha mubashara mikutano yake ya kampeni kupitia jukwaa la Twitter.
Hata hivyo, upepo ulibadilika ghafla baada ya tukio la Trump kunusurika katika jaribio la kuuawa Julai, mwaka jana. Musk akatangaza rasmi kuwa upande wake.
NINI HATIMA YAKE?
Trump ameonesha mara kadhaa kuwa ni ‘mzuri’ katika kuwanyoosha wakosoaji wake. Mathalan, ni hatua yake ya kuagiza uchunguzi ufanyike juu ya utawala wa mtangulizi wake, Joe Biden.
Kwa hili la sasa, tayari ameshatishia kumkomesha Musk kupitia kampuni zake za SpaceX Starlink.
“Njia rahisi zaidi ya kuokoa fedha katika bajeti yetu ni kuzivunjia mkataba na kuziondoshea ruzuku kampuni za Musk,” alisema Trump.
Kwa upande wa Musk, Chama chake kipya, America Party, kitamudu ushindani dhidi ya Trump na siasa za Marekani kwa ujumla? Ni swali gumu.
Kwa miaka mingi, siasa za Marekani zimekuwa chini ya ‘ubabe’ wa vyama viwili, Republican na Democrat.
Mwaka 1992, bilionea Ross Perot aliwahi kujaribu hiki anachokifanya Musk, yani kuwa mwanasiasa nje ya vyama viwili hivyo, lakini aliambulia asilimia 19 pekee ya kura.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img