Na Faraja Mulungu, Gazetini – DAR
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameonya kuhusu vitendo vya utapeli katika biashara ya madini jijini humo, akiwataka wafanyabiashara na wawekezaji kutumia Soko la Madini lililopo mkoani humo kuhakiki uhalisi wa madini kabla ya kufanya miamala.
Chalamila ameyasema hayo leo, Alhamisi, Novemba 19, 2026, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (TMIC), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Amesema biashara hiyo inakabiliwa na changamoto ya watu kuuza bidhaa zinazodaiwa kuwa madini halisi, lakini baadaye kubainika kuwa ni feki, hali inayosababisha baadhi ya wafanyabiashara kupata hasara.
Amesema amebaini changamoto hiyo baada ya kukutana na watu wawili kabla ya mkutano aliouzungumzia, ambapo mmoja alieleza kujivunia kuuza madini ya fedha, huku mwingine akilalamika kuwa amenunua madini hayo.
“Dar es Salaam tuna tatizo kubwa la matapeli wengi kuliza sana watu, hasa katika kuuza kinachoitwa feki,” amesema Chalamila.
Amesema Serikali imeweka mazingira ya kukabiliana na changamoto hiyo kupitia Soko la Madini la Dar es Salaam, ambalo lina teknolojia ya kisasa inayoweza kubaini uhalisi wa madini.
Amewataka wenye madini na wanaotaka kuingia katika biashara hiyo kutumia soko hilo kununua na kuuza bidhaa zao, ili kujiepusha na udanganyifu na hasara zinazoweza kujitokeza.
Akizungumzia fursa za uwekezaji katika sekta hiyo, Chalamila amesema Dar es Salaam ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha biashara na uongezaji thamani wa madini, licha ya kutokuwa miongoni mwa mikoa inayozalisha madini kwa wingi.
Amesema fursa za mkoa huo zinatokana na uwepo wa miundombinu ya usafirishaji, teknolojia na viwanda vinavyoweza kusaidia kuongeza thamani ya madini yanayotoka katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameitaja Bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege kuwa miongoni mwa miundombinu inayoweza kurahisisha usafirishaji wa madini kwenda katika masoko ya kimataifa.
“Dar es Salaam pia tumekuwa na teknolojia kubwa ya kuweza kuongeza thamani na ajira kubwa zinazoweza kupatikana katika eneo letu,” amesema.
Amesema mkoa huo uko tayari kupokea wawekezaji katika sekta ya madini, akieleza kuwa miundombinu iliyopo pamoja na mazingira ya amani na usalama ni miongoni mwa fursa zinazoweza kuvutia uwekezaji.
Akizungumzia maendeleo ya sekta hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu amesema mapato na makusanyo yatokanayo na madini yameongezeka kutoka Sh bilioni 346 mwaka 2018/2019 hadi Sh trilioni 1.39 mwaka 2025/2026 hatua inayoonyesha mchango unaozidi kuimarika wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi.
Mgalu amesema thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi pia imeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 4.12 mwaka 2024 hadi bilioni tano mwaka 2025.
Hata hivyo, amesema bado kuna umuhimu wa kuongeza uwezo wa ndani katika kusafisha na kuchakata madini ili kuongeza thamani kabla ya kuyauza katika masoko ya nje.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuchochea uanzishwaji wa viwanda, kuongeza ajira na kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali hizo.
Amesisitiza kuwa utajiri wa madini haupaswi kupimwa kwa kiasi cha madini kinachochimbwa pekee, bali pia kwa viwanda vinavyojengwa, ujuzi unaozalishwa na fursa zinazofunguliwa kwa wananchi.
Mgalu amesema Kamati itaendelea kuisimamia na kuishauri Serikali katika utekelezaji wa sera, sheria na bajeti za sekta hiyo, kwa kuzingatia ushiriki wa wachimbaji wadogo, uwekezaji wa Watanzania, utunzaji wa mazingira na masilahi ya jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
Aidha, amewataka washiriki wa mkutano huo kuhakikisha majadiliano yanazaa mapendekezo yanayotekelezeka yatakayofungua fursa zaidi za uwekezaji na kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika sekta ya madini.
Mkutano huo umewakutanisha wajumbe zaidi ya 1,700 kutoka nchi zaidi ya 50, ukiwa na kaulimbiu isemayo “Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi”.


