20.2 C
New York

Mkuyu Africa yazindua jukwaa la vijana kumiliki mali

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini-DAR

KAMPUNI ya MKUYU Africa imezindua jukwaa la Miliki Youth Club kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata elimu ya uwekezaji, usimamizi wa fedha na umiliki wa mali, ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi badala ya kutegemea ajira rasmi pekee.

Jukwaa hilo limekusudiwa kuwaunganisha vijana kutoka vyuoni na maeneo mbalimbali ya kazi ili kubadilishana uzoefu, kujifunza fursa za kiuchumi na kupata maarifa ya kutumia rasilimali walizonazo kuanzisha na kukuza shughuli za uzalishaji mali.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa MKUYU Africa, Juneid Othman, amewahimiza vijana kubadili mtazamo kuhusu mafanikio ya kiuchumi kwa kuweka mkazo katika uwekezaji na umiliki wa mali badala ya kutegemea ajira pekee.

Amesema vijana wanapaswa kuanza kujenga msingi wa kifedha mapema, hata wanapokuwa vyuoni au katika hatua za mwanzo za maisha yao ya kazi, badala ya kusubiri kupata ajira rasmi ndipo waanze kufikiria uwekezaji.

Amesema safari yake ya ujasiriamali ilianza akiwa na umri wa miaka 19, wakati akisomea uhasibu, ambapo alianza biashara ya nishati ya jua kwa mtaji wa Sh milioni tatu.

Kwa mujibu wa Juneid, biashara hiyo ilikua na kupanuka hadi katika masoko ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia, kabla ya kujikita pia katika sekta ya ujenzi na uwekezaji wa mali isiyohamishika.

Kwa sasa, anaeleza kuwa ana mali isiyohamishika zenye thamani inayokadiriwa kuwa zaidi ya Dola za Marekani milioni 30, zikihusisha miradi zaidi ya 10 ya majengo jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, mtaalamu wa biashara, chapa na masoko, Dkt. Beatrice Ndung’u, amesema kuanzishwa kwa Miliki Youth Club kunalenga kuwapatia vijana maarifa na ujuzi wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kutumia fursa zilizopo kujenga ustawi wao wa kiuchumi.

Amesema jukwaa hilo litatoa nafasi ya kujifunza kuhusu uwekezaji, usimamizi wa fedha na mbinu mbalimbali za kujenga utajiri kupitia umiliki wa mali.

Kupitia jukwaa hilo, vijana wanatarajiwa kupata maarifa kuhusu upangaji wa matumizi ya fedha, uwekaji wa akiba, uwekezaji wa muda mrefu na fursa za kujenga mitandao ya kibiashara itakayowasaidia kuanzisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Juneid akifurahia na wadau wa MILIKI YOUTH CLUB.

Related articles

Recent articles