23.5 C
New York

Wafanyabiashara waikimbia stendi ya mabilioni

Published:

Na Derick Milton, Gazetini-Simiyu

UIBUAJI wa miradi ya maendeleo usiozingatia ushirikishwaji wa wadau unatajwa kuwa moja ya sababu za kutokufanya vizuri kwa baadhi ya miradi nchini, kama ambavyo sasa inadhihirika kwa ujenzi wa stendi ya malori mjini Bariadi mkoani Simiyu.

Uchunguzi uliofanywa mjini hapa umethibitisha kwamba mradi huo uliobuniwa mwaka 2019 na Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwa ajili ya malori makubwa ya mizigo na ukatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 2.8, ni moja ya kielelezo cha miradi iliyokosa tija.

Ujenzi wa stendi hiyo ulitekelezwa na mkandarasi Mumang Trans and Construction Ltd akishirikiana na PEK Brothers Ltd wote kutokea Bunda mkoani Mara.

Stendi hiyo ilijengwa kwa ajili ya malori yote makubwa ya mizigo yanayoingia na kutoka katika mji wa Bariadi, ili ipakiwe na kushushwa eneo hilo.

Vyanzo mbalimbali vilivyozungumzia stendi hiyo, vimeeleza kuwa lengo kubwa la stendi hiyo lilikuwa ni kuondoa changamoto ya msongamano katikati ya mji, ambako kumekuwa na uholela wa kushusha na kupakia mizigo, hali inaoongeza msongamano wa magari mjini.

Msongamano huo ulisababisha mji kuwa mchafu, hivyo kulihitajika kituo maalumu cha kuhudumia malori. Pia lengo lingine lilikuwa ni kupanua mji wa Bariadi wenye takribani wakazi 55,479 ambao unaelezwa kukua kwa kasi kubwa.

Licha ya utekelezaji wa mradi huo kukamilika kwa wakati tangu mwaka 2020, hadi sasa takribani miaka sita haitumiwi kiasi cha kuigeuka kuwa mahame (limetelekezwa) kinyume cha malengo yaliyokusudiwa.

Kwa ujumla, madereva wa malori, wafanyabiashara na mawakala wa mizigo, wameisusa stendi hiyo, wakitoa sababu mbalimbali licha ya fedha nyingi za walipa kodi kutumika kugharimia ujenzi wake.

Lawama nyingi zinaekezwa kwa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwa kile kinachoelezwa ilitekeleza mradi bila ya kushirikisha wadau, inatuhumiwa kuwa ilibuni mradi ambao haukuwa shirikishi.

Ripoti ya CAG

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2025/2026, ikizungumzia mradi huo katika ukaguzi kwenye Halmashauri ya Mji wa Bariadi, inasema kuwa haukufanyika utafiti wa kutosha kabla ya kutekelezwa kwa mradi mkubwa kama huo.

Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Simiyu, Fortunatus Donge, anasema Halmashauri ilitekeleza mradi huo bila ya watalaamu wake kufanya utafiti wa kutosha kama mradi una manufaa kwa serikali na wananchi wake.

“Katika ukaguzi tulichokibaini ni kuwa mradi haukufanyiwa utafiti wa kutosha, mradi umetumia fedha nyingi za umma, lakini hautumiki, malori hayataki kupaki,” anasema Donge.

Mkaguzi huyo anasema stendi hiyo kutotumika ipasavyo ni matumizi mabaya ya fedha za umma. Anaishauri Halmashauri kubadilisha matumizi ya stendi hiyo kwa kubuni mradi mpya utakaowekezwa kwenye eneo hilo.

Ripoti ya TAKUKURU

Mbali na CAG ambaye alikagua mradi huo, nayo Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) katika ripoti yake ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kuanzia mwaka 2023 hadi 2026 imebaini mradi huo ulitekelezwa bila ya ushirikishwaji wa wadau.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Simiyu, Aron Misanga, anaeleza katika ripoti hiyo kuwa jumla ya miradi 102 yenye thamani ya Sh bilioni 63.3 ilifanyiwa ukaguzi na ufuatiliaji na ikabainika kuwa baadhi ya miradi ilitekelezwa bila jamii kushirikishwa.

“Moja mradi ambao tulibaini wadau hawakushirikishwa ni stendi hiyo ya malori, tangu umekamilika ni muda mrefu, lakini haitumiki. Wenye magari wamegoma kutumia stendi hiyo,” anasema Misanga.

Uchunguzi wa awali

Uchunguzi unaonyesha malori yanaendelea kushusha na kupakia katikati ya mji, bila kujali kutozwa faini ya Sh 100,000 kwa kuikimbia stendi mahususi kwa shughuli hiyo.

Takwimu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, zinaonyesha kuwa ni malori 5-10 ndani ya mwezi ndiyo yanashusha na kupakia mizigo ndani ya stendi hiyo.

Katika uchunguzi huo umeonyesha takribani malori 150 kwa mwezi (takwimu ambazo siyo rasmi) yanaendelea kushusha mizigo katikati ya mji kwenye maeneo ambayo siyo rasmi.

Uchunguzi huo umeonyesha maroli hayo utozwa faini (Wrong Parking) na uongozi wa Halmashauri ambapo kila gari utozwa Sh 100,000 likikutwa linashusha mizigo katika eneo mbalo siyo rasmi.

Licha ya faini hiyo, bado idadi ya malori kuendelea kushusha mizigo katikati ya mji inaongezeka kila wakati, huku stendi maalumu kwa ajili ya shughuli hiyo ikigeuka mahame (limetelekezwa).

Wafanyabiashara walia umbali

Wafanyabiashara katika Mji wa Bariadi, ambao ndiyo walikuwa walengwa wakuu wa kutumia stendi hiyo, wanatoa sababu kuu mbili ambazo zimewapeleka kutokutumia stendi hiyo.

Moja ya sababu kubwa ambayo inatolewa na wafanyabiashara kuikimbia stendi hiyo ni umbali.

Stendi hiyo imejengwa umbali wa kilometa saba kutoka katikati ya Mji, wafanyabiashara wanasema ili kuondoa mzigo kutoka iliko stendi hiyo hadi katikati ya mji, kuna gharama kubwa wanaingia.

Neema Shija ni mjasliamali ambaye anajishughulisha na biashara ya nafaka, anasema akishusha mzigo ndani ya stendi hiyo atalazimika kuingia gharama nyingine ya kusafirisha bidhaa zake hadi mjini.

“Ukiangalia mitaji yetu ni midogo sana, uwezo wa kumudu gharama mara mbili hatuna, ukishushia humo ndani, unatakiwa kutafuta gari ndogo au bajaji kuleta mzigo hadi mjini na gharama zake ni kubwa,” anasema Neema.

Naye Jumanne Singibala mfanyabiashara wa mbao, anasema wamekuwa wakikaa vikao na viongozi wa Halmashauri na Wilaya na waliwaeleza huo umbali ni hasara kubwa kwao.

“Mfano mimi nikishusha mzingo wa mbao, gari kubwa zima, itanilazimu kwa umbali huo nitumie gari ndogo ambalo litabeba zaidi ya safari 15 kuleta mzigo wote mjini,” anasema Singibala.

Mfanyabiashara huyo anabainisha kuwa gari ndogo ili ibeba mzingo kutoka kwenye hiyo stendi hadi mjini gharama zake ni Sh 40,000 hadi 50,000 kila safari moja.

“Ukiweka hizo gharama kwa mfanyabiashara inakuwa hasara kubwa sana, stendi ni nzuri, lakini imejengwa mbali sana, inakuwa ngumu kuitumia na ndiyo maana tunaendelea kushushia humu mjini katikati,” anasema Singabala.

Naye Manase Shingile anasema amewahi kutumia mara moja stendi hiyo ambapo alitumia gharama kubwa kubeba mizigo yake kutoka stendi hiyo kuupeleka mjini dukani kwake.

“Sisi wenye mizigo ya bidhaa mbalimbali, tumekuwa tukitumia pikipiki za magurudumu matatu (guta) ambapo kila safari ya kubeba mzigo ni Sh. 25,000 hadi 30,000,” anasema Shingile.

Anasema kwa mtu mwenye mzigo mkubwa italazimika kuusomba kuupeleka mjini zaidi ya safari 10 hadi mzigo umalizike, hali ambayo alieleza ni kikwazo kikubwa kwao na inawaingizia hasara kubwa.

Usalama wa mizigo ni kitendawili

Usalama wa mizigo ni kikwazo cha pili ambacho kimesababisha wafanyabiashara kuikimbia stendi hiyo.

Wanasema kuwa stendi hiyo wakati wa ujenzi wake suala la usalama wa mizigo halikuzingatiwa, hali inayowaathiri wakati wa mvua au jua kali, kwani hakuna sehemu ya kuhifadhi mizigo.

Henry Shabani mmoja wafanyabiashara anasema katika kipindi cha mvua hali ndiyo inakuwa mbaya zaidi, kwani kukosekana kwa eneo la kuhifadhia mizigo kuna hatari kubwa sana kwa mizigo yao kunyeshewa hivyo kuharibika.

“Wakati stendi inaanza kufanya kazi, tulianza kushushia uko, lakini tulipata shida sana mvua zilipoanza kunyesha, mizigo ya wafanyabiashara ilinyeshewa mvua na tukapata hasara kubwa sana,” anaeleza Shabani.

Mawakala wa mizigo walonga

Mawakala wa mizigo katika Mji wa Bariadi, nao wanakiri ugumu wa wafanyabiashara kutumia stendi hiyo kutokana na sababu kubwa mbili, ambazo ni usalama wa mizigo yao na umbali.

Jumanne Kiyumbi mmoja wa mawakala anasema kuwa hakuna mfanyabiashara ambaye yuko tayari kuona mizigo yake inanyeshewa mvua au kupigwa na jua, kutokana na stendi hiyo kukosa ghala la kuhifadhi mizigo.

Anasema asilimia kubwa ya wafanyabiashara wameikimbia stendi hiyo, na wamekuwa wakishushia mizigo yao kwenye maeneo ambayo siyo sahihi na wengine kushushia katika maduka yao.

Kiyumbi anasema kuwa hata wao kama mawakala imekuwa ngumu kufanyia kazi ndani ya stendi hiyo, kwani hakuna mfanyabiashara ambaye yuko tayari kuingia gharama mara mbili kwa ajili ya mzigo wake.

“Jambo hili limetufanya hata sisi kutangatanga kutafuta sehemu sahihi ya kushushia mizigo, kwa sasa tunafanyia kazi katika maeneo ambayo siyo rasmi hapa mjini katikati,” anasema Kiyumbi.

Julius Mlangila naye ni wakala wa mizigo anasema kutokana na wafanyabiashara kukataa kutumia stendi hiyo waliamua kuanzisha stendi bubu kwa ajili ya kushushia mizigo.

“Kila gari linalofika kushusha mzigo kwenye eneo letu jipya, Halmashauri wanachukua ushuru (faini), kila gari linalipia Sh 100,000 na wafanyabiashara wapo tayari kulipa hicho kiasi na siyo kushushia kwenye ile stendi,” anasema Mlangila.

Wakala huyo anasema kuwa kitendo cha stendi hiyo kutotumika imekuwa hasara kubwa kwa serikali, kwani mapato mengi yanapotea kutokana na wafanyabiashara wengi kushusha mizigo majumbani kwao.

“Kuna mapato mengi ya Halmashauri yanapotea kwa kiwango kikubwa, magari ambayo yanashusha mizigo kwa siku ni mengi sana, na ni baadhi tu ndiyo yanalipa ushuru na mengine hayalipi kabisa,” anasema Mlangila.

Madreva watoa ya moyoni

Jafari Mohamed ambaye ni dereva aliyekubali kuhojiwa wakati gari lake likishusha mzigo ndani ya stendi hiyo, alisema kuwa hata wao madreva, wanapata ugumu kutumia stendi hiyo kutokana na kukosa huduma mbalimbali za kijamii, pia umbali wa huduma zilizopo na ilipojengwa.

Anasema kuwa katika eneo la stendi hiyo hakuna nyumba za kulala wageni (guest house), na wala hakuna sehemu za kupata chakula kama migawaha au vinywaji mbalimbali.

“Hili eneo ni kama porini, hakuna nyumba ya kulala wageni au mgahawa wa chakula, dreva unafika hapa umechoka, inakulazima upaki gari humu ndani, kisha uchukue bodaboda kwa gharama ya Sh 5,000 ndiyo upelekwe mjini upumzike,” anasema Mohamed.

Wakubwa wa Halmashauri wafunguka

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Idd Ndabhona, anakiri stendi hiyo kutotumika huku akibainisha uongozi wake umeanza kufanyia kazi maoni na ushauri wa CAG) na TAKUKURU.

Ndabhona anasema wakati mradi unabuniwa, watalaamu waliwaza mbele zaidi kuwa mji wa Bariadi kila mwaka unakua, hivyo kutokana na hali hiyo walishauri stendi hiyo ijengwe eneo hilo.

“Kweli ni mbali, lakini huo ulikuwa ushauri wa kitaalumu ijengwe kule kutokana na mji kukua kila wakati, tuliwaza mbele zaidi ili kupunguza msongamano mjini,” anasema Ndabhona.

Mkurugenzi huyo anaeleza kuwa changamoto zote ambazo zipo kwenye stendi hiyo ikiwamo usalama wa mizigo, wamezibainisha na wanaendelea na tathimini ya mradi huo.

“Watalaamu watakaa na kupitia changamoto zote, ufanisi wa mradi kama ambavyo tumeshauriwa, kisha tutakuja na jibu kama tuibadilishie matumizi au tufanye jambo gani,” anasema Ndhabona.

Neno la Mkuu wa Mkoa

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Anamringi Macha, katika kikoa cha Baraza la Madiwani cha kujadili ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) alisema haya yeye alifanya uchunguzi na kubaini utafiti haukufanyika wa kutosha kabla ya mradi huo kutekelezwa.

Macha anasema kuwa katika uchunguzi ambao aliufanya, sababu ambazo wafanyabiashara walimweleza aliziona zina ukweli. “Suala la umbali, usalama wa bidhaa zao kwa mazingira ya hiyo stendi unaona kabisa zina ukweli,” alisema Macha.

0-0x0-0-0#

Macha alisema kuwa wadau hawakushirikishwa kabla ya mradi kutekelezwa, aliutaka uongozi wa Halmashauri kutafuta mradi mwingine ambao utatekelezwa kwenye eneo la stendi hiyo.

“Mimi nadhani ushauri wa CAG ufanyiwe kazi, mradi umekuwa hasara kwa Halmashauri, fanyeni tathmini upya kuangalia ni mradi gani mwingine unaweza kutekelezwa pale na ukaleta ufanisi kwenye halmashauri.

Related articles

Recent articles