5.3 C
New York

Koffi Olomide: Akorofishana na Debaba, aanzisha Quartier Latin International – [2]

Published:

KINSHASA, DRC

KATIKA sehemu ya kwanza, tuliishia pale Koffi alipohitimu masomo ya Chuo Kikuu na kutunukiwa Shahada ya Uchumi wa Biashara mwaka 1981, hivyo kurudi Kinshasa kwa ajili ya kuanza kutafuta ajira. Simulizi inaendelea …

Kama ilivyo kwa vijana wengi wanaomaliza masomo ya elimu ya juu, Koffi alirudi DRC na kukuta mazingira magumu ya kupata ajira. Hii ilimfanya arudi Ulaya [Ufaransa] kutafuta kazi.

Aliporejea DRC mwaka 1982 baada ya mambo kuwa magumu Ulaya, ndipo alipokutana na mkongwe Debaba, ambaye alimfikishia wazo la kuungana na kuanzisha bendi ya Historia Musica, ambayo pia iliitwa Historia Esthetique.

Hatimaye, bendi hiyo ilianzishwa mwaka 1983, ambapo Debaba akawa muanzilishi, Koffi akiwa Rais na mwimbaji, na Lele Nsundi akiwa dairekta. Iliwahusisha pia Cele Le Roi, Desouza Santu, Koko Anana Efoloko, Muzola Ngunga, Laza le Chestre, Coco Coluche, Djoe Mile, Derval, Adamo Leovis, Moreno, Athos, Autri, Commando, na Lokombe Bola Bolite.

Hata hivyo, Koffi hakudumu sana kwenye bendi hiyo, ikielezwa sababu ya kuondoka ni mgogoro wa ndani kati yake na Debaba.

Alipoiacha Historia Musica, Koffi aliamua kufanya kazi kama msanii anayejitegemea [solo artist] na kuachia albamu yake ya ‘Ngounda’ akipewa sapoti na wasanii kutoka kwa mkongwe Zaiko Langa Langa.

Ni baada ya mapokeo mazuri, aliachia albamu ya pili, ‘Lady Bo’, mwaka 1984, kipindi ambacho lejendari Zaiko Langa Langa alikwa na albamu mbili za moto sokoni, ‘Oka Biso’ na ‘Tokangi Robinet’, ambazo pia Koffi alishirikishwa.

Mwitikio wa mashabiki na mafanikio makubwa sokoni yalimfanya Koffi arejee studio na ‘kupika’ albamu yake ya tatu, ‘Diva’, aliyoachia mwaka 1985. Ni albamu iliyotengengezwa katiak studio za Madeleine mjini Brussels, Ubelgiji.

Kama ilivyuokuwa katika albamu zilizopita, Koffi aliwatumia wasanii wa Zaiko Langa Langa, akiwamo mpigaji gitaa la ‘bass’, Popolipo, na waimbaji kutoka Bendi ya Choc Stars, wakiwamo Carlyto Lassa, Debaba na Jenerali Defao.

Staili yake ya uimbaji wa taratibu na uvaaji wa mavazi ya kisasa na ya gharama viliupa mwonekano mpya muziki wa Rhumba, hivyo Koffi kujikuta akiigwa na wasanii wengi, hasa vijana.

Aliachia albamu yake ya nne, ‘Ngobila’, mwaka 1986 lakini haikufanya vizuri, ikilinganishwa na zile tatu za mwanzo. Ni mwaka huo huo, akaanzisha Bendi yake maarufu ya Quartier Latin International.

Itaendelea …

Related articles

Recent articles