MANCHESTER, Uingereza
MANCHESTER United wamemtangaza Mauricio Pochettino kuwa kocha wao mpya, ambapo Muargentina huyo amepewa mikoba ya Michael Carrick aliyefutwa kazi baada ya mwenendo mbaya wa timu hiyo msimu huu.
Pochettino [54], ametua Old Trafford akitokea kwenye majukumu ya kuinoa timu ya soka ya Taifa ya Marekani iliyoishia hatua ya 16 Bora katika fainali zilizopita za Kombe la Dunia.
Hii inakuwa klabu yake ya saba kwenye maisha yake ya kufundisha soka tangu alipoanza na Espanyol mwaka 2009. Anarejea kwenye ngazi ya klabu tangu alipoondoka Chelsea mwaka 2024.
Akiwa ameshafanya kazi Southampton, Tottenham na Chelsea kwa nyakati tofauti, uzoefu wa Ligi Kuu ya England [EPL] ni silaha nyingine kubwa aliyohamia nayo jijini Manchester.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi, kipimo chake cha kwanza ni Jumapili ya Novemba 22, ambapo atakuwa na Man United katika mchezo wa ugenini dhidi ya ‘Majogoo’ wa Anfield, Liverpool.
Je, mashabiki wa Man United watarajie nini kwa Pochettino, hasa katika mechi alizokutana na vigogo akiwa EPL enzi hizo?
ARSENAL
Katika mechi 15 alizowahi kukutana na Washika Bunduki hao wa London kwenye Ligi, Pochettino alishinda tatu, sare nane na kufungwa nne. Michezo yote mitatu aliyoshinda ni ile aliyokuwa akiinoa Tottenham.
Hata hivyo, alitandikwa mabao 5-0 na Arsenal katika mechi yake ya mwisho EPL, wakati huo akiinoa Chelsea [Aprili, 2024].
CHELSEA
Katika mechi za Ligi, amewahi kuvaana na Chelsea mara 13, ambapo alishinda tano, sare mbili na kufungwa sita. Kama si sare ya mabao 2-2 dhidi ya Blues, Tottenham yake ingeweza kutwaa ubingwa wa EPL mwaka 2016.
LIVERPOOL
Kwa miaka yote aliyodumu EPL, Liverpool ilikuwa timu ngumu zaidi kwa Pochettino. Alikutana nayo mara 16 lakini alishinda mechi tatu, sare tano na kuchezea vichapo nane. Mwaka 2019, alifungwa na Liverpool katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa.
MANCHESTER CITY
Pochettino ameshinda mara nne, ametoa sare tano na kufungwa saba katika mechi 16 za Ligi [EPL] alizokutana na Man City. Kwamba bado Man City ni moja ya timu ngumu mbele ya kocha huyo.
MANCHESTER UNITED
Akiwa EPL, Pochettino alikutana na ‘Mashetani Wekundu’ mara 15 kwenye mechi za Ligi Kuu hiyo. Katika michezo hiyo, Muargentina huyo alishinda mitano, sare mara tatu na kufungwa saba. Mwaka 2018, wakati huo akiwa Tottenham, alipoteza nusu fainali ya Kombe la FA.
TOTTENHAM
Akiwa kocha wa Southampton, Pochettino alifungwa mechi zote tatu za Ligi dhidi ya Tottenham, mbili akipoteza kwa kichapo cha mabao 3-2. Akiwa Chelsea msimu wa 2023-24, akashinda mechi zote za EPL dhidi ya Tottenham.


