LONDON, Uingereza
BAADA ya Michael Carrick wa Manchester United na Pierre Sage aliyekuwa Crystal Palace, bado kuna makocha wengine wa Ligi Kuu ya England [EPL] walio kwenye presha kubwa ya kufukuzwa kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa 2026-27.
Miongoni mwa wanaoweza kufuata nyayo ni kocha wa Sunderland, Regis Le Bris. Aliiwezesha timu hiyo kurudi Ligi Kuu lakini msimu uliopita [2025-26] walimaliza katika nafasi ya saba.
Hata hivyo, mambo ni magumu kwa ‘Black Cats’ msimu huu kwani timu iko nafasi ya 19 kwenye msimamo wa Ligi baada ya kukusanya pointi nane tu katika michezo 10.
Kocha mwingine aliye kwenye presha ya kupoteza kibarua ni Matthias Jaissle wa Newcastle United. Mjerumani huyo alipewa kazi baada ya Eddie Howe kuondoka.
Mambo hayakwenda vizuri kwake kwani sare ya bao 1-1 dhidi ya Fulham katika mchezo uliopita imeiweka Newcastle katika nafasi ya 12 kwenye msimamo, ikiwa na pointi 12 baada ya mechi 10.
Jaissle amekuwa akikosolewa pia kwa staili yake ya uchezaji wa mipira mirefu, badala ya kumiliki mpira kama ilivyokuwa Newcastle ya makocha waliotangulia, akiwamo Howe.
Aidha, Oliver Glasner wa Nottingham Forest naye anaingia kwenye mkumbo huo wa makocha wanaokabiliwa na hatari ya kupoteza kazi. Forest imekusanya pointi tisa pekee katika michezo 10, hivyo inashika nafasi ya 16 kwenye msimamo.


