Na mwandishi wetu, Gazetini
KATIKA sehemu ya tatu ya mfululizo wa makala haya, tuliona namna Idi Amin akiwa Mkuu wa Majeshi alivyopindua Serikali ya Rais Milton Obote mwaka 1971 na kuahidi mabadiliko makubwa nchini Uganda.
Wiki moja baadaye ya mapinduzi, alijitangaza kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu. Akaunda Baraza la Ushauri la Ulinzi, ambalo yeye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wake.
Kwa nafasi yake hiyo, alijaza wanajeshi katika nafasi za juu na nyeti serikalini na wengine akiwapa kuongoza mashirika ya umma.
Kwa upande wake, Obote aliukimbia mkono wa chuma wa Idi Amin na kukimbilia Tanzania, ambayo wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Julius Nyerere.
Baadaye, wakimbizi 20,000 wa Uganda nao waliingia Tanzania wakikimbia utawala wa kidikteta wa Idi Amin. Ni kundi ambalo mwaka 1972 likijaribu bila mafanikio kufanya mapinduzi ya kumng’oa Idi Amin.
Ni wakati ambao kwa Uganda, utawala wa Idi Amin uliendesha operesheni za kuwateka, kuwatesa, kuwasababishia ulemavu, na hata kuwaua wakosoaji wake.
Makundi yaliyotajwa kuumizwa zaidi na udikteta huo ni viongozi wa makabila, dini, waandishi wa habari, wasanii, wanasheria, wasomi, na raia wa kigeni waliokosoa baadhi ya mambo.
Zipo taarifa kuwa miili ya waliouawa na vyombo vya dola kwa amri ya Idi Amin ilipelekwa kwa siri na kutupwa katika Mto Nile.
Bado hakuna idadi kamili ya waliuawa kipindi hicho, ingawa vyanzo vingi vinataja idadi kuwa ni zaidi ya 300,000 hadi 500,000.
Miongoni mwa watu maarufu waliouawa na utawala wa Idi Amin kwa nyakati tofauti ni aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Jaji Mkuu, Benedicto Kiwanuka.
Pia, orodha hiyo inayo majina ya aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana, Janani Luwum, na Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Uganda,
Joseph Mubiru.
Wengine ni aliyekuwa Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Makerere, Frank Kalimuzo, mwandishi wa vitabu, Byron Kawadwa, na waliokuwa Mawaziri katika utawala wa Idi Amin, Erinayo Wilson Oryema na Charles Oboth Ofumbi.
Katika kitabu chake cha ‘State of Blood: The Inside Story of Idi Amin’ cha mwaka 1977, aliyekuwa Waziri wa Afya kwa miaka mitatu ya utawala huo, Henry Kyemba, anasema:
“Tabia ya ukatili aliyokuwa nayo Idi Amin ilitokana na aina ya kabila alilotoka. Kakwa, kama yalivyo makabila mengi ya Uganda, lilitumia sadaka ya damu kwa maadui zake.”
Kupitia kitabu hicho, ukurasa wa 109 hadi 110, Kyemba anasimulia Idi Amin alivyowahi kusema aliwahi kula nyama ya mtu.
Usikose sehemu ya tano ya makala haya … Tembelea www.gazetini.co.tz


