17.1 C
New York

Dk. Homera azindua huduma mpya za kidijitali

Published:

Na mwandshi wetu, Gazetini

WAZIRI wa Nishati, Dk. Juma Homera, amezindua Mkataba wa Huduma kwa Wateja uliohuishwa pamoja na mifumo na huduma mpya za TANESCO, katika hatua inayolenga kubadilisha namna Shirika linavyowahudumia wateja kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Uzinduzi huo uliofanyika leo, Oktoba 6, 2026, katika Ukumbi wa Super Dome, jijini Dar es Salaam, umehusisha pia uzinduzi wa Twiga Assistant, Twiga AI Chatbot, namba mpya ya 185 kwa ajili ya wateja wakubwa, Kitengo cha Wateja Wakubwa kilichoboreshwa pamoja na Premium Customer Portal.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Homera amesema matumizi ya mifumo ya kisasa yanaendelea kuiwezesha Tanesco kuboresha huduma kwa kuzingatia uwajibikaji, uwazi na weledi, huku akitaka changamoto zinazowakabili wananchi katika matumizi ya umeme kushughulikiwa kwa haraka.

Amesema huduma za umeme zina uhusiano wa moja kwa moja na shughuli za uzalishaji na uchumi, hivyo mifumo ya utoaji huduma inapaswa kwenda sambamba na mahitaji ya wananchi na kasi ya maendeleo ya sekta ya nishati.

“Mwelekeo wa Serikali ni kujenga sekta ya nishati inayoweza kuunga mkono kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Tunataka kuona shughuli za uzalishaji zinaendelea bila vikwazo visivyo vya lazima na tunataka wananchi wapate huduma kwa urahisi zaidi,” amesema Waziri Homera.

Waziri Homera amesema Tanzania hivi sasa ina uwezo wa uzalishaji wa umeme wa Megawati 4,606 dhidi ya mahitaji ya juu ya Megawati 2,316, hali inayotoa nafasi ya kukuza shughuli za kiuchumi kupitia uwekezaji katika viwanda, biashara na shughuli za kijamii.

Twiga AI kuondoa urasimu wa makaratasi

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, amesema uzinduzi wa Twiga Assistant ni sehemu ya mabadiliko ya Shirika katika namna linavyotoa huduma, kutoka mifumo inayotegemea zaidi makaratasi kwenda kwenye mifumo ya kielektroniki inayomuwezesha mteja kupata huduma kwa haraka.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza muda ambao mteja hutumia kusubiri huduma na kusogeza huduma za Tanesco karibu zaidi na wananchi.

“Tanesco imeamua kushuka chini na kusogeza huduma zake karibu na wananchi,” amesema Twange.

Kwa mujibu wa Twange, kukamilika kwa miradi mbalimbali ya kimkakati ya umeme, ikiwemo Mradi wa Chalinze–Dodoma, kunatoa nafasi kwa Shirika kuongeza nguvu katika ubunifu wa namna ya kuwafikia na kuwahudumia wateja.

Huduma mpya ni kwa mteja

Hafla hiyo iliyobeba kaulimbiu ya “EXTRA MILE” imekuja na mfululizo wa huduma mpya zinazolenga kuboresha uzoefu wa mteja.

Miongoni mwa huduma hizo ni Twiga AI Chatbot, mfumo saidizi wa kidijitali unaolenga kujibu maswali ya wateja; namba 185 kwa ajili ya wateja wakubwa; Premium Customer Portal, mfumo maalumu kwa ajili ya wateja wakubwa; pamoja na maboresho ya Kitengo cha Wateja Wakubwa.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Mhe. Balozi Zuhura Bundala, amesema Bodi itaendelea kuisimamia Tanesco ili utoaji wa huduma uendane na matumizi ya teknolojia za kisasa na kuhakikisha huduma zinamfikia mteja moja kwa moja bila vikwazo.

“Bodi itaendelea kuishauri Tanesco katika utoaji wa huduma kwa ufanisi. Kwetu sisi, mteja ni mfalme, na huduma inayotolewa na Shirika inamgusa mwananchi moja kwa moja. Tumejipanga kuhakikisha jitihada hizi zinaendelea kupiga hatua,” amesema Balozi Bundala.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Subira Mgalu, ameipongeza Wizara ya Nishati kupitia Tanesco kwa kuendelea kuja na ubunifu unaolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Uzinduzi huo umefanyika wakati wa kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, ukiashiria hatua ya Tanesco kuelekea katika utoaji wa huduma unaotumia zaidi teknolojia, huku ikilenga kumwezesha mteja kupata huduma kwa urahisi, haraka na kwa ufanisi.

Related articles

Recent articles