15.9 C
New York

Halotel yaahidi kutoa intaneti bure kwa shule nchini

Published:

Na Imani Nathaniel, Gazetini

Kampuni ya Halotel imeahidi kutoa huduma ya intaneti bure katika shule nchini, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kusaidia kukuza elimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuongeza fursa kwa wanafunzi kujifunza kwa kutumia teknolojia.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Mkurugenzi wa Viettel Group, Do Minah Phuong, wakati wa hafla ya kukabidhi kompyuta na vifaa kwa ajili ya darasa la TEHAMA katika shule ya sekondari Mbezi Inn, Dar es Salaam.

Phuong amesema mbali na kutoa kompyuta, kampuni hiyo imeiwezesha shule hiyo kwa mfumo wa kisasa wa intaneti utakaosaidia wanafunzi katika masomo ya TEHAMA.

Amesema wataendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuendeleza matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki, amesema elimu ya TEHAMA ni muhimu kwa maendeleo ya taaluma hiyo mashuleni na katika jamii.

Kairuki ameishukuru Halotel kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto za elimu, hususan katika eneo la TEHAMA.

Ameiomba kampuni hiyo kuendelea kutoa huduma hizo kwa shule mbalimbali nchini ili kusaidia kuleta mapinduzi katika elimu na mawasiliano.

Pia amewataka wanafunzi kutumia TEHAMA kwa manufaa ya maendeleo yao na jamii, huku akiwataka wadau wengine kuiga mfano huo katika kukuza matumizi ya teknolojia nchini.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kila kijana anapata elimu ya TEHAMA.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amewataka walimu na wanafunzi kutunza vifaa vilivyotolewa ili viendelee kutumika katika kukuza elimu ya TEHAMA shuleni hapo.

Related articles

Recent articles