MOSCOW, Urusi
MWANASIASA mwandamizi wa upinzani kupitia Chama cha Yabloko, Lev Shlosberg, anafahamika kwa matamko yake ya kuikosoa Serikali ya Rais Vladimir Putin.
Kati ya mambo mengi aliyoyapazia sauti ya juu ni hatua ya Rais Putin kuagiza jeshi kuivamia Ukraine. Vita hivyo vilianza Februari, 2022, na vimeendelea hadi leo hii.
Kwa mujibu wake, kitendo cha kuivamia Ukraine hakuna tafsiri nyingine zaidi ya ‘matumizi mabaya ya jeshi’ yaliyofanywa na uongozi wa Rais Putin.
Kwa sasa, Shlosberg yuko chini ya ulinzi mkali baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 11 na mwezi mmoja gerezani kwa kosa la kuichafua taasisi ya jeshi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa hakuna kosa alilofanya, na badala yake kesi hiyo ni sehemu ya siasa chafu, akisema Urusi haipaswi kukimbia ukweli, kwamba vita dhidi ya Ukraine vilivyodumu kwa miaka minne na nusu havina tija.
“Vimegharimu maisha ya maelfu ya watu wasio na hatia. Muda wowote kuanzia sasa, itatoka idadi kamili ya waliopoteza maisha, na hapo wananchi (wa Urusi) wataona vita hivyo ni vibaya kiasi gani,” alisema.
Hivi karibuni, taarifa kutoka katika moja ya vyombo vya habari vikubwa vya Urusi, Mediazona, zilidai kuwa wanajeshi wa Urusi zaidi ya 239,354 wameuawa katika vita hivyo.
Hata hivyo, vyanzo vingine vimeeleza kuwa idadi ni kubwa zaidi, ikitajwa kufikia vifo vya wanajeshi 350,000.
Kwa upande wake, Serikali ya Urusi chini ya Rais Putin imekuwa haina kawaida ya kutangaza idadi ya vifo vya wapiganaji wake kwenye uwanja wa vita dhidi ya Ukraine.
Kama hiyo haitoshi, Februari 24, 2022, Bunge lilipitisha Sheria inayoruhusu mashitaka dhidi ya yeyote anayepuuza kinachofanywa na jeshi. Adhabu ni pamoja na kifungo cha muda mrefu gerezani.
Shlosberg alikamatwa mwaka 2025 na kufunguliwa mashitaka ya kufananisha vita dhidi ya Ukraine na ‘mchezo wa damu’. Baadaye, aliongezewa kosa la kusambaza taarifa za uongo juu ya vita hivyo.
Aidha, anakuwa mwanasiasa wa pili wa upinzani ‘kupitiwa’ na Sheria hiyo baada ya Naibu wake, Maxim Kruglov, kuhukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani kwa kosa la aina hiyo.
Lakini Shlosberg na hata baadhi ya wanaharakati wanaona Sheria hiyo imezua hofu, kama si uoga, kwa wananchi na sasa wanashindwa kutoa maoni juu ya mustakabali wa nchi yao katika vita dhidi ya Ukraine.


