KABUL, Afghanistan
KWA wananchi wa Afghanistan, miaka mitano ya utawala wa Kundi la Taliban imekuwa ya mafanikio makubwa katika kurejesha amani nchini humo.
Hata hivyo, wanalitaka Kundi hilo kujikita katika kutengeneza ajira ili kuinua uchumi wa wananchi, pamoja na kuondosha utaratibu wa watoto wa kike kunyimwa haki ya kuendelea na masomo baada ya kutimiza umri wa miaka 12.
Taliban walirejea madarakani Agosti 15, 2021 baada ya Marekani na NATO kuondosha vikosi vyake vya kijeshi katika Taifa hilo la Kiarabu.
Kabla ya hatua hiyo, Afghanistan ilikuwa kwenye vita kwa miaka zaidi ya 20, ambapo Taliban walikuwa wakipigana na wanajeshi wa Marekani na NATO.
Kwa sasa, hali ya usalama imeimarika. “Asante Mungu, miaka mitano imepita kwa amani,” anasema Mohammad Qasim, mkazi wa Kabul mwenye umri wa miaka 30.
“Ni matumaini yetu sasa Serikali itatengeneza fursa nyingi za ajira kwa ajili ya vijana na kuhimiza umuhimu wa elimu.”
Wakati inaingia madarakani mwaka 2021, Taliban iliahidi kuwaruhusu wanawake kupata elimu, jambo ambalo halijatekelezeka hadi leo hii.
Muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani, ilitangaza kuwa kiwango cha mwisho cha mtoto wa kike kusoma ni darasa la sita na ni marufuku kufika chuo kikuu.
Baadaye, wanawake walipigwa marufuku kuingia gym, kwenye maegesho ya magari, kujihusisha na michezo, na kusafiri umbali mrefu bila msimamizi (mwanaume).
Hata hivyo, licha ya Taliban kusema imejenga uhusiano na mataifa 40 kwa miaka mitano, bado Urusi ndiyo nchi pekee inayoitambua Serikali ya Taliban.
Kwa upande mwingine, Programu ya Chakula ya Umoja wa Mataifa (UNWFP), Afghanistan chini ya Taliban ina idadi kubwa ya watoto wenye utapiamlo.
Wakati huo huo, yapo madai ya nchi hiyo kukabiliwa na uhaba wa wataalamu katika kada muhimu za udaktari na ukandarasi.


