28.2 C
New York

Dk. Samia kuzindua JNHPP Agosti 22, mchango wake wafikia 44.9% gridi ya taifa

Published:

Na Mwandishi wetu, Gazetini

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) Agosti 22, 2026, katika eneo la mradi Rufiji, Mkoa wa Pwani, katika hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi uwezo wa Tanzania kuzalisha na kusambaza umeme wa uhakika.

JNHPP ni miongoni mwa miradi mikubwa na ya kimkakati katika historia ya sekta ya nishati nchini, ikiwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115. Kituo hicho kimejengwa kwa gharama ya takribani Sh trilioni 7.452, fedha zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.

Akizungumza leo Jumamosi, Agosti 15, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema ujenzi wa mradi huo ulianza Juni 2019 na kukamilika Machi 2025, huku ukiwa umeajiri takribani wafanyakazi 12,000 wakati wa ujenzi.

“Mradi huu umegharimu takribani Shilingi trilioni 7.452, fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania,” amesema Ndejembi.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi.

Amesema uwezo wa mitambo yote ya kuzalisha umeme nchini umefikia takribani MW 4,646, huku JNHPP pekee ikichangia MW 2,115, sawa na karibu nusu ya uwezo huo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, tangu kuanza kuzalisha umeme, JNHPP imeendelea kuongeza kiwango cha umeme kinachoingia katika Gridi ya Taifa, hatua iliyosaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa umeme na mgao katika maeneo mbalimbali nchini.

“Takwimu zinaonesha kuwa hadi Mei 31, 2026, JNHPP ilikuwa imezalisha takribani asilimia 44.9 ya jumla ya umeme uliozalishwa na kuingia katika Gridi ya Taifa katika kipindi cha mwaka mmoja,” amesema.

Mbali na uzalishaji wa umeme, Ndejembi amesema bwawa la JNHPP lina uwezo wa kuhifadhi takribani mita za ujazo bilioni 33 za maji, kiasi kinachokadiriwa kuwa mara 10 ya uwezo wa Bwawa la Mtera.

Amesema hifadhi hiyo inaongeza umuhimu wa mradi katika sekta nyingine, ikiwamo kilimo cha umwagiliaji, utalii na matumizi ya maji kwa binadamu.

Kwa mtazamo wa kiuchumi, uwepo wa umeme wa uhakika unatarajiwa kuongeza uzalishaji viwandani, kukuza biashara na kuvutia uwekezaji, huku ukipunguza athari za upungufu wa nishati kwa shughuli za uzalishaji.

default

JNHPP pia ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuimarisha miundombinu ya nishati na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Uzinduzi wa Agosti 22 unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika historia ya sekta ya nishati Tanzania, huku JNHPP ikiendelea kutazamwa kama nguzo ya kuongeza uwezo wa Taifa wa kuzalisha umeme na kuweka msingi wa uchumi unaotegemea nishati ya uhakika.

Related articles

Recent articles