Na mwandishi wetu, Gazetini
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche, amewataka wanachama wa chama hicho kuongeza kiwango cha kujitolea katika harakati za kisiasa, akisema kufanya hivyo kutawapa nguvu viongozi na wanachama wanaobeba gharama kubwa za kupigania mabadiliko nchini.
Akizungumza na wanachama wa Chadema mkoani Shinyanga Agosti 5, 2026, Heche alisema wananchi wengi wanaendelea kukabiliwa na changamoto za kiuchumi, huku baadhi wakishindwa kumudu hata mahitaji ya msingi kama gharama za matibabu, ada za masomo na kodi ya nyumba.
“Kuna mtu mtoto wake anamfia kwa shilingi 3,000 kwa sababu hawezi kumpeleka hospitali. Kuna mwanafunzi wa chuo anakutumia ujumbe akikuomba umsaidie Shilingi 50,000 baada ya kuzuiwa kufanya mitihani. Haya ndiyo maisha ya Watanzania wengi,” amesema Heche.
Amesema hali hiyo ndiyo inayowapa wajibu viongozi na wanachama wa Chadema kuendelea kupigania mabadiliko, akisisitiza kuwa mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila kujitoa kwa dhati.
“Siku mkigundua na kutambua kuwa kazi hii si kwa ajili ya John Heche wala Tundu Lissu, mkajitoa hata robo ya jinsi mnavyojitolea kwenye mambo mengine mnayoona ni muhimu, tutabadilisha nchi. Lakini bila kujitoa tutakuwa tunawakatisha tamaa watu,” amesema.
Heche amesema viongozi na wanachama wengi wamekuwa wakitoa sadaka kubwa kwa ajili ya chama, ikiwemo kukamatwa, kufungwa na kukabiliwa na changamoto mbalimbali, lakini wakati mwingine hukata tamaa wanapoona juhudi zao hazipati ushirikiano unaostahili kutoka kwa wanachama.
Akimzungumzia Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Heche amesema viongozi wanaopitia mateso kwa ajili ya harakati za kisiasa wanahitaji kuungwa mkono na wanachama badala ya kukatishwa tamaa.
“Lissu anakamatwa, anakaa gerezani kwa muda mrefu. Baadaye anarudi anakuta mtu ambaye amekuwa akimpigania hana ushirikiano. Sisi sote ni binadamu, watu wanaweza kukata tamaa wanapoona wanajitolea lakini hawapati sapoti ya kutosha,” alisema.
Ameongeza kuwa wapo viongozi wanaokataa maslahi binafsi na kuweka maisha yao rehani kwa kile alichodai ni maslahi ya wananchi, hivyo ni wajibu wa wanachama kusimama pamoja nao katika harakati za chama.
Aliwahimiza wanachama wa Chadema mkoani Shinyanga kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama kwa moyo wa kujitolea, akisema kufanya hivyo kutaimarisha harakati za kisiasa na kuongeza ari ya viongozi na wanachama wanaoendelea kujitolea kwa ajili ya kile alichosema ni mapambano ya kuleta mabadiliko nchini.
“Tufanye kazi hii kwa moyo ule ule tunaoufanya katika shughuli zetu nyingine. Tukijitoa kwa pamoja, tutawapa nguvu wale wanaopigania mabadiliko na tutafikia malengo yetu,” amesema Heche.


