28.4 C
New York

Mwamba wa ‘unga’ aliyeisumbua Marekani kwa miaka 40

Published:

LOS ANGELES, Marekani

ANAITWA El Mayo. Ndilo jina maarufu zaidi kuliko Ismael Zambada alilopewa na wazazi wake, akiwa pia ndiye muasisi wa genge hatari la biashara ya dawa za kulevya la Sinaloa huko Mexico.

Kwa sasa, El Mayo (76), anatumikia kifungo cha maisha gerezani nchini Marekani lakini haikuwa rahisi kunasa kwenye mtego wa ICA (Shirika la Ujasusi la Marekani).

Sambamba na hukumu hiyo ambayo imewekewa pia kipengele cha kutokupewa msamaha wa rais, ametakiwa kulipa faini ya Dola za Marekani bilioni 15.

Hiyo inakuwa hukumu kubwa zaidi kwa kiongozi wa makundi ya uhalifu nchini Mexico tangu Marekani ilipomkamata Joaquin Guzman ‘El Chapo’ na kumfunga kifungo cha maisha mwaka 2019.

ALIVYOKAMATWA

Baada ya miongo minne (miaka 40) ya kutafutwa, El Mayo alikamatwa Julai, 2024, nchini Mexico na kusafirishwa hadi Texas, Marekani, kwa ajili ya kusomewa mashitaka yake.

Mahakama nchini Marekani ilijiridhisha kuwa aliasisi na kuliongoza Kundi la uhalifu la Sinaloa, ambalo linajihusisha na biashara ya dawa za kulevya, kuteka na kutesa watu, pamoja na ujambazi.

Waendesha mashitaka wa Marekani walidai kuwa El Mayo aliongoza matukio ya kikatili, ikiwamo kumuua mtoto wa dada yake. Vilevile, kupitia mtandao wake mkubwa wa dawa za kulevya, El Mayo aliingiza tani nyingi za cocaine nchini Marekani.

Hukumu ya kusota gerezani kwa kipindi chote cha maisha yake ilikuja baada ya El Mayo kukutwa na hatia katika mashitaka takribani 85. “Ismael Zambada Garcia alitumia miongo minne kuikwepa Marekani na kupata faida ya mabilioni ya dola na kuua kila aliyepita mbele yake,” alisema Mwanasheria Joseph Nocella Jr.

AJUTIA, AOMBA RADHI

Kwa upande wake, El Mayo aliieleza Mahakama kujituia kwa vitendo vya uhalifu, akiomba radhi kwa matukio yake na kuwataka vijana kutokuiga mwenendo wake wa maisha.

Aidha, alisema mazingira aliyozaliwa na kukulia nchini Mexico ndiyo chanzo cha kuingia kwenye matukio ya uhalifu. “Nilikulia katika mazingira ambayo vurugu na uhalifu vilikuwa vitu vya kawaida, lakini nafahamu hiyo haiwezi kuwa kisingizio.

“Kuna kipindi kinafika kila mtu anatakiwa kuwajibika kwa maamuzi aliyofanya. Sikuzingatia, na vitendo vyangu viliwagharimu wengi,” alisema El Mayo kuiambia Mahakama.

Ni kwa kukiri kwake kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na makosa yote yaliyotajwa, Mahakama ikamsamehe hukumu ya kifo.

UHUSIANO WAKE NA EL CHAPO

Akiwa na El Chapo, walianzisha genge la uhalifu la Sinaloa katika miaka ya 1980, ambalo baadaye liliitikisa dunia, ikiwamo Marekani, kwa mtandao wake mkubwa wa dawa za kulevya, utekaji, mauaji, na ujambazi.

Hata El Mayo alipokamatwa mwaka 2024, alikuwa na mtoto wa El Chapo, Joaquin Guzman Lopez ‘Chapitos’, ambaye naye ana mashitaka ya dawa za kulevya, ingawa bado hajahukumiwa.

Ripoti zinaeleza kuwa Chapitos ndiye ‘aliyemchoma’ El Mayo baada ya kumtaka wakutane eneo ambalo tayari lilikuwa na polisi wa Marekani na Mexico.

Tangu kukakamatwa kwake, Sinaloa limegawanyika makundi mawili, kila moja likitaka kushika uongozi. Mvutano huo umezalisha matukio mengi ya kurushiana risasi, kama ilivyotokea baada ya El Chapo kukamatwa mwaka 2016.

Related articles

Recent articles